UMOJA wa Jamii ya Watu kutoka nchini India Bengali wa Dar es Salaam (Bango Sangho) wametoa huduma za afya bure kwa watoto wa chini ya miaka mitano eneo la Kibugumu lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Zaidi ya watoto 100 wamepatiwa huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma za vipimo na ushauri, huduma za afya ya kinywa na meno na pia kufanyiwa ukaguzi na ushauri wa lishe suala ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa familia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Mratibu wa huduma hizo, Dk. Ali Mzige ambaye ni daktari wa watoto amesema Bango Sangho wameamua kuendesha zoezi hilo ili kuwasaidia baadhi ya familia ambazo zimekuwa zikipata changamoto kwa magonjwa anuai yanayowashambulia watoto.
Alisema zoezi hilo limeendeshwa bure chini ya uratibu wa Umoja wa Jamii ya Watu wa India, Bengali ikiwa ni utaratibu wao wa kujitolea kusaidia jamii katika masuala mbalimbali yanayowakabilia. Alisema mbali ya huduma za vipimo ushauri na huduma za kliniki wazazi pia walipewa ushauri stahiki wa kiafya kwa watoto wao ili kukabiliana na magonjwa nyemelezi yanayowaathiri watoto.
Akifafanua zaidi juu ya zoezi hilo, Dk. Mzige alisema idadi kubwa ya watoto waliopatiwa huduma eneo hilo wamebainika kuwa na upungugu wa wekundu wa damu pamoja na upungufu wa uzito jamboa ambalo linaathiri hali ya ukuaji wao kiafya.
Alisema waliobainika kuwa na matatizo makubwa kiafya wamepewa rufaa kwenda hospitali za juu kwa msaada zaidi wa kiafya. Alisema pamoja na mambo mengine wanawashauri wazazi kuwatairi mapema iwezekanavyo watoto wa kiume ili kuzuia uwezekano wa kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo.
“…Kwa watoto wa kike tunawashauri mama zao wawasafishe mara kwa mara wanapojisaidia…wengine wanafunga pampasi lakini inakaa muda mrefu inakuwa na unyevu jamboa ambalo linaweza kumsababishia mtoto kupata UTI…maambukizi kwenye njia ya mkojo kwa hiyo hili ni suala ambalo wazazi tunawaelekeza ili kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa watoto,” alifafanua Dk. Mzige.
Aidha alisema mtoto anapopata maambukizi ya mara kwa mara yanamuathiri katika ongezeko la uzito na kukosa hamu ya kula jambo ambalo ni hatari kiafya kwa watoto wengi. Miongoni mwa madaktari waliokuwa wakitoa huduma hizo ni pamoja na wataalamu wa afya ya kinywa na meno, madaktari wataalamu wa watoto pamoja na wataalamu wa vipimo vya maabara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bango Sangho Dar es Salaam, Amit Nandi alisema wameamua kutoa huduma hilo eneo la nje ya Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma za afya bure na karibu jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama na mzigo kwao.
Alisema huduma hizo za afya huzitoa kila mwaka bure kwa jamii ikiwa ni mchango wao kwa jamii ya kawaida ili nayo iweze kupata huduma za afya ambazo zimekuwa changamoto hasa maeneo ya vijijini na nje ya miji. Jamii ya Bango Sangho pia wamesaidia ujenzi wa shule ya msingi na awali ya Kibugumu ikiwa ni mchango kwa jamii.