KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
“Uchaguzi wa mwaka 2015 ni uthibitisho wa wazi na dhamira ya muda mrefu ya Watanzania kwa demokrasia, amani na utulivu. Nina imani kuwa masuala ya uchaguzi yaliyobakia yatashughulikiwa kupitia taratibu za kisheria zilizopo kwa njia ya amani na uwazi.” Bw. Ban Ki Moon alisema kwenye barua yake ya pongezi ambayo amemtumia Rais Dk. Magufuli.
Bw. Ban Ki Moon alisema anaamini kuwa, chini ya uongozi wa Dk. Magufuli, Serikali ya Tanzania itashughulika na juhudi za kuondoa umaskini, kuimarisha utawala bora na kuendeleza juhudi za Tanzania katika kupigania amani na utulivu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na nje zaidi ya Ukanda huu.
“Napenda kukuhakishia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kukuunga mkono pamoja na Serikali yako katika juhudi hizi”. Mhe. Ban Ki Moon amesema.
Katibu Mkuu Bw. Ban Ki Moon pia ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenza imara na wa kutumainiwa na Umoja wa Mataifa kwa miongo yote.
“Nathamini ushirikiano uliopo baina ya Umoja wa Mataifa na nchi yako na katika kuendeleza malengo ya UN, nakutakia mafanikio katika kutekeleza shughuli zako”. Bw. Ban Ki Moon amesema katika salamu zake.