TANZANIA na Marekani zimeimarisha mahusiano yao katika kipindi cha miaka minne iliyopita kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri wa balozi anaemaliza muda wake nchini Alfonso Lenhardt.
“Asante kwa kazi nzuri uliyoifanya katika kipindi chote cha miaka minne uliyoitumikia hapa Tanzania. Mambo mengi na makubwa yenye kuleta maendeleo na manufaa kwa Tanzania yamefanyika hapa nchini na umeyasimamia na kuyafanikisha ipasavyo”.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemueleza Balozi Lenhardt leo alipofika Ikulu kuaga na kumshukuru Rais na serikali yake kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha ubalozi hapa nchini.
Rais Kikwere amesema ushirikiano wa nchi hizi mbili umekua na kuimarika zaidi na anatarajia kuwa balozi ajaye naye atakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano baina ya nchi hizi. Naye balozi Lenhart amesema Tanzania iko moyoni mwake na ataendelea kuwa balozi wa Tanzania popote alipo.
“Nikushukuru wewe mheshimiwa Rais na serikali yako kwa ushirikiano mzuri na utayari wa kunisikiliza na kunisaidia wakati wote nilipohitaji ushauri wako, umekuwa msaada mkubwa kwangu. Asante kwa ushirikiano wako na siku zote nitaendelea kuwa balozi wa Tanzania kwani Tanzania iko moyoni mwangu”.
Mapema Balozi Lenhardt alipata nafasi ya kumtakia Rais Kikwete siku njema ya Kuzaliwa na kumpatia zawadi kama kumbukumbu ya siku hii ya leo na mara baada ya mazungumzo Rais na balozi wakapata nafasi ya kula chakula cha mchana pamoja na mama Salma Kikwete na Mama Jacqueline Lenhardt, ambaye ni mke wa balozi Lenhardt.