Balozi wa China amwaga sifa Tanzania

Balozi mpya wa China nchini Tanzania, Lu Youqing (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu uongozi wake nchini Tanzania na vipaumbele katika kuimarisha ushirikiano na kuleta maendeleo ya Tanzania na China. Wengine kutoka kushoto ni Fu. Jijun Mshauri wa Masuala ya Siasa ubalozi wa China na Hu Changming (kulia) ambaye ni Mshauri Mwandamizi wa Uhusiano wa ubalozi huo. Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.

Na Aron Msigwa–MAELEZO, Dar es Salaam

BALOZI mpya wa China nchini Tanzania, Lu Youqing ameahidi kutumia muda wa uongozi wake kuwatumikia raia wa China na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ushirikiano uliopo kati ya mataifa hayo kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii unadumishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za ubalozi huo leo jijini Dar es Salaam amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kufuatia maendeleo na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanatokea duniani.

Amesema China ikiwa ni nchi ya pili duniani kwa maendeleo itaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali katika bara la Afrika kuimarisha na kutetea amani, umoja, kushiriki katika utatuzi wa migogoro mbalimbali inayotokea katika nchi za Afrika na kusaidia nchi marafiki katika mipango ya maendeleo.

“Hivi sasa uchumi wetu unakua kwa kasi sana na kufikia pato la taifa la dola za kimarekani trilioni 7.5 kwa mwaka sawa na asilimia 9.2 maendeleo haya ni makubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa maendeleo yaliyopo nchini China kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na mfumo na sera nzuri za uchumi zilizopo pamoja na mabadiliko ya wananchi kifikra na kitabia na kuongeza kuwa kuna juhudi mbalimbali zilizofanywa katika kuinua uchumi wa China zikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi, uzingatiaji wa masuala ya ajira, matumizi ya sayansi na teknolojia na utoaji wa elimu bora kwa wananchi.

Katika kuhakikisha kuwa ushirikiano baina ya China na Tanzania unaendelezwa katika nyanja mbalimbali balozi Lu amesema katika kipindi cha uongozi wake nchi yake itaendelea kuchangia kutoa nafasi za ajira kupitia makampuni mbalimbali ya kichina na miradi mbalimbali inayoanzishwa nchini Tanzania katika sekta ya kilimo, mawasiliano, utengenezaji wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara, madaraja na ujenzi wa mitandao ya mawasiliano.

“Kihistoria tuna ushirikiano mkubwa sana baina ya Tanzania na China katika miradi mbalimbali inayoanzishwa pamoja na miradi ya ushirikiano ya reli ya Tazara na kiwanda cha Urafiki,” amesema Balozi Lu.

Ameongeza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja ya elimu katika utoaji wa ufadhili na nafasi za masomo kwa watanzania kwenda nchini humo kujifunza masuala mbalimbali na kuongeza kuwa nchi yake itaendelea kutoa fursa kwa wasanii mbalimbali waliopo nchini kwenda China kujifunza masuala mbalimbali ili kuboresha kazi zao na tasnia ya sanaa kwa ujumla.