Na.Aron Msigwa – MAELEZO.
1/9/2015.Dar es salaam.
Katibu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wahandisi nchini Tanzania itakayofanyika Septemba 3 hadi 4 jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya sherehe hiyo Prof.Bakari Mwinyiwiwa amesema Kuwa Jumuiya ya Wahandisi nchini Tanzania inafanya maadhimisho hayo kwa mara ya 13 toka kuzinduliwa kwake mwaka 2003 kuenzi mchango wa wahandisi katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuwawezesha waajiri na wahandisi wazalendo na watumiaji wa huduma za kihandisi kutambua uwezo wa wahandisi wazalendo na kampuni zao pia kuwahamasisha wanafunzi wa kitanzania wanaosomea fani hiyo ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatajikita katika kuangalia masuala mbalimbali ya maendeleo hasa ujenzi wa miundombinu,Maendeleo ya viwanda, ukuzaji wa uwezo, na maendeleo ya shughuli za kilimo nchini Tanzani.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini Muhandisi Steven Mlote ameeleza kuwa wakati wa maadhimisho hayo shughuli mbalimbali za kitaaluma zitafanyika ikiwemo majadiliano ya kina kuhusu shughuli za kihandisi nchini na miaka 15 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Amesema wakati wa maadhimisho hayo kutakuwa na utambuzi na utoaji wa Tuzo na zawadi mbalimbali kwa wahandisi na wahitimu wa Taasisi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao mwaka 2014/2015 pamoja na wahandisi kurejea kiapo cha utii kwa taaluma yao.
Ameongeza kuwa wakati wa maadhimisho hayo kutakuwa na maonesho ya kiufundi ya jumuiya za wahandisi wa Tanzania kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia St.Joseph na Chuo cha Ardhi (ARU).
Jumuiya nyingine ni ile ya Makandarasi ,Kampuni za Ushauri wa kihandisi,Mashirika na makampuni ya kibiashara na taasisi za utafiti.