Balozi Mteule wa Vietnam Akabidhi Hati Ikulu

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Vietnam hapa nchini, Vo Thanh Nam huko Ikulu hapa Dar es Salaam tarehe 4.11.2013. Rais Kikwete baadaye anaonekana akifanya mazungumzo na Balozi huyo. (PICHA NA JOHN LUKUWI)

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Vietnam hapa nchini, Vo Thanh Nam huko Ikulu hapa Dar es Salaam tarehe 4.11.2013. Rais Kikwete baadaye anaonekana akifanya mazungumzo na Balozi huyo. (PICHA NA JOHN LUKUWI)

IMG_6582
Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Balozi Mteule wa Vietnam hapa nchini, Vo Thanh Nam huko Ikulu hapa Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Novemba 4, 2013, amepokea Hati za Utambulisho za Mheshimiwa Vo Thanh Nam, Balozi mpya wa Vietnam katika Tanzania. Katika mazungumzo yaliyofuatia baada ya Balozi huyo kuwasilisha Hati za utambulisho katika tukio lililofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete amesema kwamba Tanzania na Vietnam zimekuwa nchi marafiki kwa miaka mingi lakini bado iko haja ya kupandisha kiwango cha urafiki na ushirikiano huo.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inapenda kujifunza kutoka Vietnam jinsi gani nchi hiyo ilivyoweza kufanya mageuzi makubwa na ya haraka katika sekta ya kilimo.

“Mmefanya maajabu ya kuigwa na dunia katika kilimo kwa maana ya kuongeza tija na uzalishaji. Kiasi cha miaka 10 iliyopita, Vietnam tayari ilikuwa nchi iliyokuwa inaongoza duniani kwa uzalishaji wa mpunga na ilikuwa inashikilia nafasi ya pili duniani katika uzalishaji wa zao jipya la kahawa nchini humo baada ya Brazil.”

Naye Balozi Vo Thank Nam amemwambia Rais Kikwete kuwa mwezi ujao nchi hiyo italeta ujumbe maalum ambao utakuja kujadiliana na Tanzania jinsi gani ya kushirikiana kwa karibu zaidi katika kilimo na shughuli za umwagiliaji na kutiliana saini makubaliano kuhusu suala hilo.

Aidha, Balozi huyo amemwambia Rais Kikwete kuwa Shirika la Mawasiliano ya Simu la Vietnam la Viatel liko tayari kuwekeza kiasi cha dola za Marekani milioni 20 katika Kampuni ya Simu Tanzania ya TTCL ili kuimarisha kampuni hiyo kama makampuni hayo yatafikia makubaliano kuhusu ushirikiano kati yao.