Balozi Mahiga Ampokea Mkuu Mpya wa Shirika la UN Kuendeleza Viwanda Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga (kulia) akimpokea Mkuu wa Shirika la Kuendeleza Viwanda la Umoja wa Mataifa-UNIDO, Dr. Stephen Kargbo alipowasili kukabidhi hati ya utambulisho ofisi za Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Kuendeleza Viwanda la Umoja wa Mataifa-UNIDO, Dr. Stephen Kargbo (wa pili kulia) alipowasili kukabidhi hati ya utambulisho ofisi za Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.

 

Picha ya pamoja ya Balozi, Mwakilishi na maofisa kutoka Wizarani na Umoja wa Mataifa.

Na Stella Vuzo

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga leo amepokea hati za utambulisho za mwakilishi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuendeleza viwanda nchini Tanzania (UNIDO) wizarani kwake jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Mahiga alisema kiongozi huyo, aitwaye Dr. Stephen Kargbo kutoka nchini Sierra Leone, anakuja wakati muafaka ambapo Tanzania imetangaza mkakati wa kuendeleza viwanda.

Kwa upande wake, Dk. Kargbo alimweleza Balozi Mahiga kuhusu miradi mbali mbali ambayo tayari inatekelezwa na shirika la UNIDO nchini ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme mdogo kupitia maporomoko ya maji madogo vijijini –(mini hydroelectric power plants)na ushirikiano uliopo baina ya chuo cha wahandisi (COET) katika kutengeneza vifua umeme(turbines). Balozi Mahiga alipongeza jitihada zinazoendelezwa na kuelezea kwamba Tanzania ina matarajio makubwa kwamba itafanya kazi na kiongozi huyo wa shirika la kuendeleza viwanda la Umoja wa Mataifa nchini.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Balozi Mahiga alifafanua kwamba, “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa miaka mitano ijayo umeainisha mikakati mitano ya kusaidia kendeleza viwanda nchini Tanzania ikiwemo kuwezesha wizara na taasisi mbalimbali kuwa na ujuzi wa kutosha, kuwezesha vijana wa Tanzania kupata mafunzo hapa nchini na huko nje na pia taasisi zetu kama veta kuzidisha ufanisi.”

Maeneo mengine yaliyolengwa ni pamoja na, “kuanzisha viwanda vidogo vidogo hasa vya nishati ili kuwezesha viwanda vya vijijini na mikoani,kushughulikia suala zima la uwekezaji kutoka nje na jinsi Tanzania inavyoweza kujenga mkakati na kuainisha mkakati wake na wawekezaji kutoka nje na la mwisho ni kuwa na uhusiano wa kuona kwamba viwanda vitakavyoendelezwa katika kipindi hiki vinapata masoko duniani na vijana wana uwezo wa kusimamia mikakati yetu ya viwanda.”

Mwakilishi huyo mpya Naye mwakilishi wa UNIDO nchini, Dk. Stephen Bainous Kargbo aliwaeleza wanahabri kwamba, “hii ni siku ya muhimu kwangu kuwasilisha hati za utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa lakini zaidi inahusu viwanda, kwani hii ni ajenga kuu ya Serikali na tunafurahia muda huu muafaka kwa shirika la UNIDO kufanya kazi na serikali katika kuendeleza viwanda.”

Afisa huyo aliambatana na Afisa kutoka ofisini kwake, Bw. Gerald Runyoro ambaye alisema UNIDO imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba ili kusiaidia vijijini, “inashiriki katika kuzalisha umeme kupitia miradi ya maporomoko ya maji madogo na tunaunganisha umeme hata kwenye gridi ya taifa.” Runyoro alielezea pia kwamba UNIDO inazalisha nishati ya majumbani ya kupikia ikiwa na lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira.

“UNIDO inatoa elimu na ujasiriamali hasa kwa wafanyabishara wadogo wadogo hasa wale wanaoingia katika kuongeza thamani kwenye bidhaa na vilevile kuwa na namna ya kuzifungasha vizuri na kuweza kuzitafutia masoko hapa nchini na nje ya nchi.” Alisema Bwana Runyoro.

Tanzania imekuwa nchi mwanachama wa UNIDO tangu 1985 na shughuli nyingi za shirika hili zimelenga kuongeza ujuzi wa taasisi mbalimbali kuwa na sera za viwanda na takwimu sahihi, kujenga ushindani wa viwanda, kuhamasisha nishati na mazingira endelevu,na viwanda vidogo vya kilimo. UNIDO imesaidia wataalamu wa viwanda kama vya ngozi miongoni mwa viwanda vingine nchini.

Dr. Stephen Bainous Kargbo, analeta nchini ujuzi wa zaidi ya miaka thelathini katika masuala mbalimbali ya maendeleo na amefanya kazi katika nchi mbalimbali duniani.