Mwandishi Maalum
BALOZI wa Umoja wa Afrika nchini Marekani Bi. Amina Salum Ali ametunukiwa tuzo ya Mwanadiplomasia wa Mwaka na Taasisi ya Jumuiya za Africa jimbo la Michigan nchini Marekani. Balozi Ali alitunukiwa tuzo hiyo katika sherehe kubwa iliyoandaliwa na Muungano wa Jumuiya za Waafrika kwenye jimbo hilo iliyofanyika katika jiji la Detroit nchini Marekani usiku wa Oktoba, 2011. Balozi Ali alikuwa ndiye mgeni wa heshima kwenye tafrija hiyo iliyosindikizwa kwa mapambo, mavazi, muziki na burudani zenye maudhui ya mila na desturi mbalimbali za kiafrika
Sherehe hizo zilikuwa zikiadhimisha miaka kumi tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo ambayo inawakilishi Waafrika wapatao zaidi ya 75,000 wanaoishi katika jimbo hilo. Pamoja na tuzo kwa Balozi Ali, jumuiya hiyo ya United African Communities Organization (UAC) ilitoa pia tuzo kwa Waafrika mbalimbali ambao wameweza kutoa mchango kwa wananchi wa Waafrika waishio katika jimbo la Michigan. Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Maono katika Uongozi ilienda kwa Dr. Geoffrey Kemoli Segala raia wa Kenya mwenye kutoa huduma yake kwenye mji wa Southfield, Michigan.
Katika hotuba yake ya kupokea tuzo hiyo Balozi Amina (Tanzania) alizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Waafrika wanaoishi Marekani na haja ya Umoja wa Afrika (AU) kutafuta suluhisho la kudumu la baadhi ya changamoto hizo.
Mojawapo ya mipango ya Umoja wa Afrika kushughulikia changamoto mbalimbali ni kuitishwa kwa Kongamano Maalum litakalozungumzia masuala ya Waafrika walio nje ya bara la Afrika. Kongamano hilo kwa mujibu wa Balozi litafanyika huko nchini Afrika ya Kusini mwezi Mei, 2011 na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi za Kiafrika.
Kwa mujibu wa Balozi Amina Ali viongozi wa Afrika watakapokutana huko Afrika Kusini watazungumzia kati ya mengi jinsi ya kuja na Makubaliano ya Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na raia wao walioko nje ya bara la Afrika. Baadhi ya mambo ambayo yataguswa kwenye makubaliano hayo yatahusiana na suala la uraia wa nchi mbili, uwekezaji, wasomi kulikimbia bara la Afrika na masuala mengine ambayo Waafrika nje ya Bara la Afrika (Diaspora) wamekuwa wakitaka viongozi wao kuyashughulikia.
Balozi Amina Ali ni Mwakilishi wa Kudumu wa Jumuiya ya Afrika nchini Marekani. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo kuliwakilisha Bara la Afrika nchini Marekani na kupeleka utambulisho wake kwa Rais George W. Bush mwaka 2007 na hivyo kuwa Balozi wa kwanza wa Jumuiya ya Afrika nchini Marekani. Mojawapo ya majukumu yake ni kushirikiana na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali za Afrika nchini Marekani katika kufuatilia mambo mbalimbali katika serikali ya Marekani
Balozi Amina Ali amekuwa kwenye utumishi wa umma kwa zaidi ya miaka thelathini sasa akifanya kazi mbalimbali katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na pia katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya Ubalozi alikuwa ni Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais Zanzibar.