Na Jennifer Chamila- Maelezo
BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) limeviomba vyombo vya dola kuendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio la kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Imamu na waumini wa Kiislamu wakiwa msikitini wakati wa swala ya Idd-el-Fitri iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa.
Aidha baraza hilo limesikitishwa na kitendo hicho, na kuvitaka vyombo hivyo kuhakikisha kwamba wahalifu wote wanafikishwa mbele ya sheria. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa kwa vyombo vya habari na Mufti wa Tanzania Sheikh Issa Simba, imelaani kitendo hicho na kusema watu waliofanya kitendo hicho wamegeuka maagizo ya ya Qur’an Tukufu pamoja na Sheria za Nchi.
“BAKWATA imewataka wananchi wote kufuata taratibu sahihi jambo lolote linapo tokea.” Kama yupo mtu yoyote ana manung’uniko au hoja yoyote dhidi ya mwenzake au taasisi yoyote, ni lazima watumie taratibu sahihi za kidini au za kisheria na sio kuchukua sheria mkononi” alisema Sheikh Issa. Alisema baraza hilo linamuomba Mwenyezi Mungu awaponye watu wote waliathirika na tukio hilo.