Na Eleuteri Mangi
SERIKALI imepanga kutumia zaidi ya trilioni 19.6 ambayo ndiyo sura ya bajeti katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya nchi. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alipokuwa akiwasilisha taarifa ya sura ya Bajeti kuu ya Serikali inayotarajia kuanza kutumika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 2014/2015 jana jijini Dar es Salaam.
Waziri Saada alisema kuwa mfumo wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaoanza unazingatia sera za bajeti kwa mwaka 2014/2015 ambazo zitazingatia vipaumbele vya mpango wa Maendeleo wa Taifa na malengo ya utekelezaji wa mkakati wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Kwa upande wa matumizi ya kawaida Serikali inatrajia kutumia zaidi ya trilioni 14.2 ambayo inajumuisha mfuko mkuu wa serikali, mishahara ya watumishi wa Serikali, wizara, mikoa, halmashauri, taasisi na wakala za Serikali.
Aidha, kwa matumizi mengine yatakuwa ni kwa ajili ya maendeleo kwa mwaka wa fedha unaotarrajiwa kuanza Julai mwaka huu ambapo kiasi cha 5, 445.10 ambazo ni sawa na asilimia 27.7 zimepangwa kutumika kwa kuhusisha fedha za ndani na za nje ya nchi.
Waziri Saada akiwasilisha taarifa yake kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge hao waliipokea Taarifa ya Serikali kuhusu Makadirio ya Bajeti katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam ambayo inatarajiwa kuongeza wigo wa wabunge kuijadili bajeti hiyo kabla ya kusomwa bungeni mjini Dodoma.
Shabaha ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni kuhakikisha pato la taifa litakuwa kwa asilimia 7.2 mwaka 2014, asilimia 7.4 mwaka 2015, asilimia 7.7 mwaka 2016 na kuendelea kuongezeka hadi kufikia asilimias 8.0 ifikapo mwaka 2017. Misingi ya bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2014/2015 ni pamoja na kuendelea kuwepo na kuimarishwa amani, usalama, utulivu na utengamano misingi ambayo itasaidia kupatikana kwa katiba mpya kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Stephen Wasira akiwasilisha rasimu ya mpango wa maendeleo wa taifa katika bunge likikaa kama kamati alisema kuwa maeneo ya vipaumbele yanalenga miradi ya kitaifa ya kimkakati inayolenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi inajumuisha miundombinu ya uasfirishaji kama reli, barabara, bandari, na usafiri wa anga.
Vipaumbele vingine ni nishati, huduma ya maji mijini na vijijini, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu na huduma za kiuchumi kama fedha, biashsra na utalii.
Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda amewaasa wabunge wote washiriki kikamilifu katika kamati pamoja na serikali ili ipatikane bajeti yenye tija kwa taifa na wabunge waikamilishe kizalendo kwa kujali nchi yao. Kikao cha Bunge la bajeti kinatanguliwa na kamati mbalimbali zitakutana ambapo vikao vilianza Aprili 27, 2014 kwa wajumbe kuwasili jijini Dar es salaam na kuhitimishwa Mei 4, 2014 na wabunge kuanza safari kwenda Dodoma tayari kwa kuanza kikao chake kama ilivyopangwa.
Kamati ya bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wakati wa Bunge la bajeti, kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kamati ya Nishati na Madini, kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC) kujadili hesabu zilizokaguliwa za Serikali kuu na mashirika ya umma, kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Na nyingine ni kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kamati ya kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI, kamati ya LAAC Dar es salaam na kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamii.