Bajeti ya Serikali Yapitishwa Rasmi Bungeni

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya


BAJETI ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, imepitishwa na Bunge, huku kwa mara ya kwanza Mbunge wa Vunjo Augustine Mrema akiipinga, lakini wabunge watatu wa upinzani waliiunga mkono.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema bajeti hiyo ilipita kwa asilimia 83 baada ya kupigiwa kura za ndiyo na wabunge 219. Dk Kashililah alisema jumla ya wabunge 294 walipiga kura na kati ya hao 74 walipiga kura za hapana, huku Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi hakuamua.

Mbunge wa Vunjo (TLP) Augustine, tofauti na bajeti nyingine za serikali zilizopita ambazo alikuwa akiziunga mkono, kwa mara ya kwanza jana aliipinga bajeti hiyoAkielezea sababu ya kuipinga katika viwanja vya Bunge, Mrema alisema amefanya hivyo kwa sababu bajeti ya mwaka huu haijatatua matatizo ya wapiga kura wake wa Vunjo.

Kwa upande wa mwingine wapinzani watatu John Shibuda (Maswa Magharibi-Chadema), John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), wao walipiga kura ndiyo kwa bajeti hiyo. Shibuda mara baada ya kupiga kura hiyo ya ndiyo, alisikika akisema, “mimi ni mgombea binafsi nina maamuzi yangu huru.”

Hata hivyo wabunge 59 wa CCM akiwemo Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na wabunge wengine watatu wanaowania kuteuliwa na CCM kuwania urais, hawakupiga kura katika zoezi ya kupitisha bajeti ya mwaka 2015/2016.
Wabunge waliokosa kupiga kura ni Luhaga Mpina (Kisesa), Hamisi Kigwangalla, (Nzega) na William Ngeleja (Sengerema).

Hali kadhalika, mawaziri na manaibu watatu hawakupiga kura ambao ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Charles Kitwanga na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anna Malecela.

Akihitimisha hoja yake, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema baada ya kusikiliza michango ya wabunge bungeni, serikali imeongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Sh50,000 hadi Sh100,000. Alisema ongezeko hilo la asilimia 100, litaanza kulipwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu kwa wastaafu hao.

“Sambamba na kuongeza pensheni tutaimarisha mifumo ili kuhakikisha wazee wetu hawapati usumbufu na badala yake wanapata fedha zao huko waliko,”alisema. Alisema pia alisema Serikali itawachukulia hatua watumishi wakorofi ambao wamekuwa wakisababisha usumbufu kwa wastaafu hao.

Pensheni kwa wazee wote
Saada alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 jumla ya wazee waliopo nchini ni milioni 1.2. Alisema kuna wazee ambao katika miaka mitatu watakuwa wamefikia umri wa kupewa pensheni hiyo ambao hawakuwepo katika sensa hiyo.

“Kama tukiamua kutoa Sh10,000 kwa kila mzee kwa mwezi zinahitajika Sh140Bilioni,”alisema.

Alisema katika mwaka huu wa fedha wametenga fedha kwa ajili ya watumishi wa serikali kuwatambua wazee walipo na mfumo utakaowawezesha kufikiwa na pensheni hiyo bila usumbufu. Alisema wamekuwa na tatizo la wastaafu kutofikiwa na pensheni zao kutokana na mifumo na watumishi wasio waaminifu. Saada alisema kwa kushirikiana na benki wameweza kubaini Sh6 Bilioni zilipotea kutokana tatizo hilo.

Ongezeko la Tozo Saada aliwataka Watanzania kuchangia maendeleo yao na kuacha kulichukulia ongezeko la Sh100 kwa kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kama agenda ya kisiasa. Alisema katika utafiti waliofanya umeonyesha kuwa matumizi ya mafuta ya taa vijijini yamepungua.

Alisema utafiti huo ulibainisha kuwa mwaka 2010 mafuta ya taa yalikuwa yakitumika lita milioni 1.8 kwa siku lakini hivi sasa matumizi hayo yameshuka hadi kufikia lita 130,000 kwa siku. “Hii inamaanisha kuwa wameondokana na matumizi ya mafuta ya taa na kuanza kutumia nishati nyingine,”alisema.

Alisema jumla ya Sh276Bilioni zitakazopatikana kutokana na tozo hizo zitatumika katika kupeleka umeme na maji vijijini. Alisema Sh90Bilioni zitakwenda katika miradi ya maji vijijini na kinachobaki kitakwenda katika umeme.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz/