Bajeti 2011/2012, daladala kuumia, pombe, sigara juu tena

Na Said Mwishehe, Dodoma

BAJETI ya fedha ya mwaka 2011/2012 imeonesha kutoa matumani makubwa kwa mwananchi wa kawaida kutokana na dhamira ya Serikali kupunguza ukali wa maisha huku ikitangaza vipaumbele vyake ni umeme, maji, miundombinu, viwanja vya ndege, kuinua kilimo cha umwagiliaji na kupanua ajira.

 Katika bajeti hii mpya Serikali inatarajia kutumia zaidi ya trilioni 13.5 ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi ya ile ya mwaka 2010/2011 ambapo ilitumia trilioni 11.1; bajeti ambayo ilipingwa na wabunge wa upinzani jambo ambalo halikufua dafu dhidi ya uwingi wa wabunge wa chama tawala.

Akisoma bajeti hiyo jana bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema kiujumla bajeti imelenga kupunguza ukali wa maisha kwa Mtanzania, kwa kuangalia kodi na tozo ambazo zimekuwa zikichangia kupanda kwa gharama za vitu mbalimbali muhimu.

“Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za uchumi pamoja na misingi na sera za bajeti, sura ya Bajeti inaonesha kwamba jumla ya shilingi bilioni 13,525.9 zinahitajika kutumika katika kipindi cha 2011/12.

Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo akionyesha mkoba wenye hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12 kwa waandishi wa habari jana mjini Dodoma

 Alisema Serikali inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya sh. bilioni 6,775.9, sawa na asilimia 17.2 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni sh. bilioni 350.5. Kadhalika, kukopa kiasi cha sh. bilioni 2,475.9…,” alisema Mkulo.

Alisema kutoka kwa washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia bajeti kupitia misaada na mikopo ya jumla ya sh. bilioni 3,923.6. na kati ya fedha hizo, sh. bilioni 869.4 ni misaada na mikopo ya kibajeti huku sh. bilioni 3,054.1 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikijumuisha mifuko ya kisekta.

Katika bajeti hiyo pamoja na mambo mengine, Serikali imeendelea kuwakamua watumiaji sigara na bia kwa kuongeza kodi ukilinganisha na ile ya mwaka wa fedha uliopita; huku kwa watakaofanya makosa ya barabarani sasa kutakiwa kulipa sh. 300,000 badala ya sh. 20,000.

“Kumekuwepo na changamoto ambazo zinahitaji hatua za maksudi kuchukuliwa na wadau ikiwemo Serikali, sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja ili kupunguza makali ya maisha kwa mwananchi.

“Kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma nchini pamoja na mambo mengine inasababishwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia. Kutopatikana kwa umeme wa uhakika nalo ni tatizo lingine pamoja na upungufu wa chakula nchini. Hivyo Serikali itachukua hatua za kukabiliana na hiyo,” alisema Mkulo.

Akifafanua namna ya kupunguza ukali wa maisha Mkulo alisema bajeti ya mwaka wa 2011/2012 imeangalia maeneo mbalimbali muhimu na kuyafanyia marekebisho kwa maslahi ya Taifa ambapo, ili kupunguza bei ya mafuta, Serikali imeamua kufanya mapitio ya namna ya kuondoa tozo zinazotozwa na mamlaka mbalimbali kwa lengo la kupunguza kodi.

Waziri Mkulo alisema Serikali inakamilisha taratibu za ununuzi wa mafuta kwa wingi kwa lengo la kuyauzia kampuni ya usambazaji kwa bei ya jumla kufanya yatakavyo. Kanuni zitatoa muongozo katika uagizaji mafuta kwa pamoja zimekamilika na utaratibu huo unategemea kuanza kati kati ya mwaka wa fedha wa 2011/2012.

“Utaratibu huu unatarajiwa kupunguza bei na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo. Pamoja na juhudi hizi za Serikali, sekta binafsi inahimizwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya kutumia gesi kama nishati mbadala wa mafuta ya petroli hasa mijini. Ni matarajia yangu hatua hizi zitaleta unafuu wa bei ya mafuta na hivyo kupunguza gharama za maisha,” alisema Mkulo.

Mkulo alisema nchi inakabiliwa na upungufu wa nishati ya umeme kutokana na kiwango kidogo cha uzalishaji. Kwa kuzingatia kuwa umeme una umuhimu wa kipekee katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali itachukua hatua kadhaa za kukabiliana na tatizo hili ikiwemo kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 100 Dar es Salaam na megawati 60 Mwanza, miradi itakayo punguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.

Serikali pia imepanga kuliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupata mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa kwa ajili ya kununulia mitambo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji; pia kushirikisha sekta binafsi eneo hili kwa lengo la kuiachia TANESCO kujikita kwenye eneo moja ambalo ina uwezo nalo kujenga ushindani.

Mkulo alisema kutokana na kukamilishwa kwa sera, sheria na kanuni za ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, Serikali itaandaa utaratibu wa kuhusisha sekta binafsi kwenye suala zima la umeme; ikiwa ni pamoja na baadhi ya miradi ya umeme kutekelezwa kwa njia ya ubia.

Udhibiti Fedha za umma

Sera za matumizi ya Serikali zinalenga katika kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, yakijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika miradi ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea  kudhibiti ulimbikizaji wa madeni.

Vipaupaumbele

Mkulo alisema miunombinu ya barabara, reli, bandari na mkongo wa taifa zimetengwa sh. bilioni 2,781.4 ikilinganishwa na sh. bilioni 1,505.1 ya mwaka wa fedha uliopita, nishati na madini imetengwa sh. bilioni 539.3 ikilinganishwa na sh. bilioni 327.2, maji sh. bilioni 621.6 ikilinganishwa na sh. bilioni 397.6, kilimo na umwagiliaji sh. bilioni 926.2 ikilinganishwa na sh. bilioni 903.8 mwaka uliopita na elimu imetengewa sh. bilioni 2,283.0 ikilinganishwa na sh. bilioni 2,045.4.

Kodi za Vinyaji, Sigara juu

 Hata hivyo katika bajeti hiyo ya fedha licha ya Serikali kutoa msamaha wa kodi katika pembejeo za kilimo na kupunguza ushuru katika mafuta mazito sh. 80 hadi sh. 40. kwa upande mwingine imendelea kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 50 badala ya 120, kwenye mifuko ya plastiki.

Wakati upande wa vinjwaji baridi kutoka sh. 63 hadi sh. 69, bia inayotengenezwa na nafaka imeongezeka kutoka sh. 226 kwa lita hadi sh. 249 wakati bia nyingine zote kutoka sh. 382 hadi sh. 420 kwa lita.

Vinywaji vikali kutoka sh. 1,812 kwa lita hadi sh.1,993, huku kodi kwa sigara zisizo na kichungi kupanda kutoka sh. 6,209 hadi sh. 6,830 na sigara zenye kichungi kutoka sh.14,649 hadi sh.16,114, wakati sigara nyingine zenye sifa tofauti kutoka sh. 26,604 hadi sh. 29,264 kwa sigara elfu moja kila tozo.