Moja ya bajaj za kubebea wagonjwa ambazo zimenunuliwa nje ya nchi na Serikali. Bajaj kama hizo na zinazosemekana kuwa bora zaidi zinatengenezwa sasa Tanzania.
Na Joachim Mushi
BAJAJ maalumu za kubebea wagonjwa zenye magurudumu matatu, ambazo Serikali ya Tanzania hivi karibuni imeamua kuzitumia kubebea wagonjwa kutokana na kuwa na gharama ya chini sasa zimeanza kutengenezwa Tanzania.
Kampuni ya Comprint International Ltd ndio kwa sasa imeanza kuzitengeneza majaji hizo ambazo zinauwezo mkubwa kiubora ukilinganisha na zile zinazotoka nje.
Akizungumza na gazeti hili jana Dar es Salaam kwenye maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa, Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo, Rashid Abubakar alisema wameanza kuzitengeneza ambulance hizo za magurudumu matatu, huku zao zikiwa na ubora zaidi ukilinganisha na zinazotoka nje.
Alisema bajaj hizo wanazozitengeneza zinauwezo wa kustahimili hali mbaya ya miundombinu ya barabara vijijini huku zikiwa na mashine maalumu ambazo zinauwezo wa kupita kwenye matope na hata maeneo ya miinuko mikali bila kukwama.
Alisema bajaj zao zimetengenezwa na kujaribiwa katika miundombinu ya barabara mbaya za Tanzania hivyo kuweza kuhimili hali zote za miundombinu hiyo. Alisema kampuni yao inauwezo wa kutengeneza bajaj 1,000 kwa mwezi mmoja. Hata hivyo alisema kwa sasa bado vifaa ambavyo havitengenezwi nchini wanaviagiza kutoka nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania imeanza kuzitumia bajaj za kubebea wagonjwa kutoka nje ya nchi, ambapo imepanga kununua bajaj 400 kwa ajili ya kuzisambaza hospitali zake anuai zilizopo maeneo mbalimbali hasa vijijini.
Kutengenezwa kwa bajaj hizo kunaweza isaidia Serikali ya Tanzania kutumia vifaa hivyo kwa ajili ya hospitali za nchini, ambazo zimekuwa zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa magari ya kubebea wagonjwa. Kwa mujibu wa Abubakar alisema gharama ya bajaj moja inafikia dola 700.