Bado Morogoro Hijatangazwa Fursa za Uwekezaji –Mkuu wa Mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajab Rutengwe (kulia) akimkaribisha Balozi wa Afika ya Kusini Nchini, Bw. T. D. Mseleku  alipomtembelea Ofsini kwake  hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajab Rutengwe (kulia) akimkaribisha Balozi wa Afika ya Kusini Nchini, Bw. T. D. Mseleku alipomtembelea Ofsini kwake hivi karibuni.

Na Andrew Chimesela, Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajab Rutengwe (kulia) akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Balozi wa Afrika Kusini Bw. T. Mseleku.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajab Rutengwe (kulia) akiwa katika mazungumzo na mgeni wake Balozi wa Afrika Kusini Bw. T. Mseleku.

MKUU wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajab Rutengwe amesema pamoja na kuwa Mkoa wa Morogoro una maeneo makubwa ya ardhi bado maeneo hayo hayajatumika ipasavyo na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza mkoani humo katika Sekta ya kilimo, Viwanda na Utalii. Dk. Rutengwe ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa mazungumzo baina yake na Balozi wa Afrika ya Kusini Nchini Tanzania Mhe T. D. Mseleku alipomtembelea Ofsini kwake.

Aidha, alimueleza Balozi Mseleku kuwa eneo ambalo halijatumika kikamilifu katika Sekta ya kilimo ni kilimo cha umwagiliaji ambacho kwa Mkoa wa Morogoro kinawezekana kutokana na Mkoa kuwa na mito mingi inayotitirisha maji kipindi chote cha mwaka.

Dk. Rutengwe alisema, kwa jumla Mkoa wa Morogoro una maeneo makubwa, yenye rutuba na yanayofaa kwa kilimo. Hata hivyo alibainisha kuwa ipo ardhi kubwa inayomilikiwa na Wananchi ambao baadhi yao wameshindwa kuiendeleza na Serikali iko katika mchakato wa kuyachukua maeneo hayo na kuyatoa kwa wawekezaji watakayoyaendeleza.

“Morogoro tuna ardhi kubwa na yenye rutuba lakini haijatumika inavyotakiwa, Serekali ipo mbioni kubadilisha matumizi ya maeneo hayo ili kuwapa wawekezaji wanaoweza kuitumia ardhi hiyo kikamilifu kwa faida ya wanaMorogoro na taifa,” alisema Dk. Rutengwe.

Kuhusu kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza Mkoani Morogoro, alisema Mkoa unaandaa kongamano la Uwekezaji ambalo linatarajiwa kufanyika hivi karibuni kongamano litakalojumuisha Mikoa ya Morogoro na Pwani. Kwa upande wake Balozi wa Afrika ya Kusini Mseleku alimshukuru Dk. Rutengwe kwa kuonesha ushirikiano na dhamira ya dhati ya kuwakaribisha wawekezaji na kuomba kuendeleza ushirikiano wa pande hizo mbili uliokwishaanza.

Katika hatua nyingine Dk. Rutengwe mara kadhaa amekuwa akishawishi watendaji katika Mkoa wa Morogoro kuutangaza Mkoa kupitia vyombo vya Habari na mitandao mbalimbali ya kijamii kama Blogs ili kuharakisha maendeleo ya Mkoa na watu wake kiuchumi na kijamii.