MCHUNGAJI mstaafu Ambilikile Mwasapila (Babu) amesema baadhi ya watu wanaodai kutibu kwa kutumia tiba ya kikombe kama anavyofanya yeye ni wauaji, wezi na wanasumbuliwa na njaa, hivyo amewataka wananchi wawapuuze.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Jijini Mwanza, Aprili 13 mwaka huu,
Mwasapile alisema watu walioibuka baada ya yeye kuanza kutoa huduma ya tiba ya
kikombe wanasumbuliwa na njaa kutokana na tamaa ya fedha wanayoionesha.
Babu alitoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari kutaka atoe maoni yake juu ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara tangu kujitokeza yeye na kudai nao wanatibu magonjwa sugu kwa kutumia dozi ya kikombe kama anayotoa yeye kijijini Samunge.
Alisema watu hao wanaoibuka katika maeneo mbalimbali ya nchi wakidai kutoa tiba
ya kikombe na wengine kutumia bilauri mbili si wa kweli na wauaji na kinachowasumbua ni
njaa na tamaa ya fedha walionayo.
“Unanisikia hao ni wezi tu, wanasumbuliwa na njaa, ni njaa tu inawasumbua ni
wauaji wa watu na watauwa watu,” alisema Babu Mwasapila akitoa ufafanuzi kuhusu
tiba yake kwa waandishi wa habari waliofika kijijini kwake Samunge Loliondo ili
kujua changamoto anuai zinazomkabili pamoja na masuala mengine.
“Sina ushirikiano na mtu yeyote katika kutoa huduma ya tiba ya
kikombe maeneo mengine, dawa hii nilioteshwa na Mungu na sipaswi kuhama kwenda kutoa tiba hiyo nje ya hapa. Nilioteshwa nikaambiwa watakuja watu kutoka mabara ya Afrika, Ulaya na Asia
kupata dawa na bado nahimiza waje,” alisema Babu.
Hata hivyo aliwataka wananchi nchini kote kujihadhari na wezi na matapeli
wanaoibuka hisi sasa na kuwalaghai maeneo anuai kuwa wanaponya kwa kutumia tiba ya kikombe kama ilivyo kwake, hivyo kushauri watu wenye matatizo waende Samunge kupata dawa kwani si
mali yake bali Mungu badala ya kwenda kwa matapeli.
Naye Mratibu wa tiba ya kikombe inayotolea na Babu, Fredrick Nsajile alikemea vitendo vya rushwa katika vituo na vizuizi vya kuruhusu watu na magari yanayokwenda kwa babu Loliondo kwani ni kinyume cha maandiko ya Mungu.
Alisema katika vituo na vizuzi vilivyowekwa barabarani kuruhusu watu wanaofuata
huduma ya tiba ya kikombe cha babu kumekuwa kuna tuuma za utoaji wa rushwa ili waruhusiwe jambo ambalo alidai linamchukiza Mungu.
Alisema kuna tuhuma kuwa kituo kilichopo wilayani Bunda wameanza kuruhusu watu kwenda Loliondo baada ya kuwatoza rushwa, kudai wanao ushahidi kwamba magari zaidi ya matatu yamekuwa yakiingia kijijini hapo na kurudi, huku mengine yakiwa yanasubiri kituoni.