Kahama
WANANCHI wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo Ukimwi wameshauriwa kuendelea kutumia dawa wanazopewa na wataalamu hospitalini hata kama wamefanikiwa kunywa kikombe cha dawa ya Mchungaji Ambilikile Mwasapila.
Ushauri huo ulitolewa jana mjini hapa na Meneja wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali (SHIDEPHA+), Venance Muzuka linalojishughulisha na kuhudumia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwa na watoto yatima pamoja na wazee wasiojiweza wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake jana mjini hapa, Muzuka alisema jumla ya watu wapatao 1869 wanaoishi na VVU wanahudumiwa na shirika hilo ambapo saba kati yao wamekunywa kikombe cha ‘Babu’ hali iliyowalazimu kupima Afya zao baada ya mwezi mmoja tangu watumie dawa hiyo lakini bado wamekutwa na maambukizi.
”Mimi nimewaruhusu watu saba kutoka katika mikono yangu na wakaenda kunywa kikombe hicho na baada ya kurudi na kukaa kwa muda wa mwezi mmoja walipima katika kituo hiki hiki na kujikuta maambukizi ya Ukimwi yameongezeka tena kwa kasi kubwa na hali hii ni hatari sana kwani wanaweza kuongeza maambukizi hayo kwa watu wengine wasipojilinda,” alisema Muzuka.
Alisema baadhi ya wagonjwa wanaokunywa kikombe cha dawa hiyo wamekuwa wakiamini kuwa wamepona hivyo kusitisha kutumia dozi ya dawa wanazopatiwa na wataalamu wa afya za kupunguza makali ya Ukimwi na kutibu magonjwa mengine.
Kufuatia hali hiyo Muzuka aliwashauri wananchi wote kwa jumla kuendelea kutumia dawa wanazopewa na wataalamu wa afya kutoka katika vituo mbalimbali huku akisisitiza kulinda afya zao kwa kuepuka kupata maambukizi mapya ya VVU.
Hata hivyo pamoja na mchungaji huyo kuendelea kutoa dawa hiyo ameendelea kusisitiza wagojwa kuendelea kutumia dozi ambazo walikuwa anazozitoa inaponesha kulingana na imani ya mgonjwa