Baba Mzazi Ambaka Mtoto Wake wa Kike wa Miaka Sita

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP-Robert Boaz

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP-Robert Boaz

Na Yohane Gervas, Rombo

POLISI wilayani Rombo inamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Martini Shayo (71) mkazi wa Kijiji cha Mengeni Chini Wilaya ya Rombo kwa kosa la kumbaka mwanaye wa kike mwenye umri wa miaka sita.

Mkuu wa Polisi (OCD) wa Wilaya ya Rombo, Ralph Meela akizungumza na mtandao huu alisema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 18, 2013 majira ya saa saba mchana katika Kijiji cha Mengeni Chini Tarafa ya Mengwe wilayani hapa.

Aidha aLISEMA mtoto aliyefanyiwa ukatili huo ambaye jina lake limehifadhiwa alipata maumivu makali sehemu zake za siri hivyo baada ya polisi kupata taarifa hizo walimwandikia PF3 na kwenda kupatiwa matibabu katika hospitali ya Huruma.

Mke wa mtuhumiwa, Anna Shayo ambaye pia ni mama wa mtoto aliyebakwa amesema kuwa mume wake alimwita mwanae amfuate ndani lakini baada ya muda mfupi alimsikia akiwa anapiga kelele na alipomfuata ndani alimkuta baba akiwa anamfanyia mwanae kitendo hicho.

Aidha ameongeza kuwa baada ya hapo alipiga ukunga kuomba msaada na kutoa taarifa kituo cha polisi ambapo polisi walifika na kumkata mtuhumiwa mara moja na kumuweka chini yaulinzi. Kwa mujibu wa mtoto aliyebakwa amesema kuwa baba yake alikua na mazoea ya kumchezea wakati mama yake hayupo na kisha alikua akimpa pipi ili asiseme kwa mama yake.

Tukio hilo limeibua hisia tofauti tofauti kwa wakazi wa Rombo huku wengine wakilihusisha na imani za kishirikina na kuomba vyombo vya dola kulifanyia uchunguzi wa kutosha ili kudhibiti kabisa matukio hayo.