Baa la njaa limekwisha Somalia

Njaa ilivyotikisha nchini Somalia

UMOJA wa Mataifa (UN) umetangaza kuwa baa la njaa nchini Somalia lililotangazwa kulikumba taifa hilo hivi karibuni sasa limefikia kikomo.

Umoja huo umesema hali imeimarika nchini humo kutokana na mavuno mazuri na misaada ya kibinadamu inayoendelea kutolewa. Taarifa ndani ya Somalia zinasema; mwezi uliopita mshiriki mkuu wa shughuli za umoja huo nchini Somalia, Mark Bowden alisema maelfu ya watu wamekufa tangu mwezi Julai mwaka 2011 kutokana na baa la njaa.

Ofisa Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Jose Granziano amesema mvua kubwa iliyonyesha pamoja na misaada ya kibinadam iliyotolewa imechangia pakubwa kuimarika kwa hali ya maisha nchini Somalia.

Amesema maisha ya watu wengi yameokolewa lakini akaonya kuwa ikiwa mvua inayotarajiwa kunyesha tena haitatosha, basi hali hiyo hiyo huenda ikarelejea tena katika kipindi cha majuma kadhaa.

Watu bado wanaendelea kufa kutokana na athari za ukame huo na vita. Zaidi ya watoto elfu mia moja wanakabiliwa na tishio la kuangamia kutokana na utapia mlo. Amesema utafutaji wa suluhu ya mzozo wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili nchini Somalia utachanga pakubwa kuimarika kwa hali ya maisha nchini humo.
-BBC