Azamu Yaisambaratisha Panone Fc na Kutinga Robo Fainali FA CUP

azam

Na; Binzubeiry.co.tz

AZAM FC imekamilisha idadi ya timu nane za kucheza Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation, kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Panone FC jioni ya jana Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Kilimanjaro.

Azam FC inaungana na Yanga, Simba, zote za Dar es Salaam, Ndanda FC ya Mtwara, Coastal Union ya Tanga, Geita Gold ya Geita, Mwadui FC ya Shinyanga na Prisons ya Mbeya kutinga Nane Bora ya Kombe la Azam Sports Federation 2016.

Haikuwa kazi nyepesi kwa Azam FC kushinda mchezo wa jana, kwani walilazimika kutoka nyuma kwa bao 1-0 na kuibuka kifua mbele kwa 2-1 baada ya dakika 90 na nne za nyongeza kufidia muda uliopotezwa.

Panone walitangulia kwa bao bao la kichwa la beki wake wa kati, Godfrey Mbuda aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki kulia, Ayoub Masoud dakika ya 48.

Ni bao ambalo mabeki wa Azam FC hawawezi kukwepa lawama, kwani mfungaji aliruka peke yake na kumtungua kipa Aishi Manula.
Hata hivyo, beki Serge Wawa Pascal akafuta makosa ya safu ya ulinzi kwa kuisawazishia Azam FC dakika ya 64 akimalizia kwa kichwa kona ya beki wa kulia, Erasto Nyoni.

Nyoni tena akaenda kuchonga kona maridadi dakika ya 77 ambayo iliwababatiza mabeki wa Panone baada ya kutemwa na kipa wao, Mansoor Mansoor kabla ya kumkuta mshambuliaji Mkenya, Allan Watende Wanga aliyeifungia Azam FC bao la ushindi.

MATOKEO HATUA YA 16 BORA KOMBE LA TFF
Jana; Februari 29, 2016
Panone FC 1-2 Azam FC (Ushirika, Moshi)
Februari 28, 2016
Simba SC 5-1 Singida United (Taifa, Dar es Salaam)
Toto African 0-1 Geita Gold (Kirumba, Mwanza))
Februari 24, 2016
Yanga SC 2-1 JKT Mlale (Taifa, Dar es Salaam)
Februari 26, 2016
Ndanda FC 3-0 JKT Ruvu (Nangwanda, Mtwara)
Coastal Union 1-0 Mtibwa Sugar (Mkwakwani, Tanga)
Februari 27, 2016
Mwadui FC 3-1 Rhino Rangers (Mwadui, Shinyanga)
Prisons 2-1 Mbeya City (Sokoine, Mbeya)

Azam FC inaungana na Yanga, Simba, zote za Dar es Salaam, Ndanda FC ya Mtwara, Coastal Union ya Tanga, Geita Gold ya Geita, Mwadui FC ya Shinyanga na Prisons ya Mbeya kutinga Nane Bora ya Kombe la Azam Sports Federation 2016.