Azam Sasa Mambo Safi, Wahispania Washika Usukani

IMG_20160516_140803

UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, tayari umefikia makubaliano na wakufunzi kutoka nchini Hispania, Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Mtaalamu wa Viungo, Jonas Garcia.

Makocha hao wawili waliotua nchini Ijumaa iliyopita, kila mmoja amesaini mkataba wa mwaka mmoja kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho msimu ujao wakirithi mikoba ya Mwingereza Stewart Hall, aliyeachia ngazi pamoja na benchi lake zima la ufundi alilokuja nalo Juni mwaka jana.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, jana amethibitishi kuwa ni rasmi sasa benchi la ufundi la timu hiyo litakuwa na sura mpya msimu ujao kwa makocha kutoka nchini Hispania.

“Tayari tumeshafikiana nao makubaliano na kila mmoja amesaini mkataba wa mwaka mmoja, kocha mkuu atakuja na benchi lake zima la ufundi kama ilivyokuwa kwa kocha aliyepita (Stewart Hall),” alisema.

Bosi huyo aliyebobea kwenye mambo ya uongozi wa soka, aliongeza kuwa mbali na makocha hao, wengine watakaoongezeka baadaye ni Kocha Msaidizi namba moja, Kocha Msaidizi namba mbili ambaye ataendelea kuwa mzawa Dennis Kitambi, Daktari wa timu pamoja na Kocha wa Makipa.

Mara baada ya makocha hao kusaini mkataba tayari wameanza rasmi kazi ya kukisimamia kikosi hicho ambacho kwa sasa kitaendelea kuwa chini ya Dennis Kitambi hadi kumalizika kwa msimu huu.

Kitambi atakiongoza kikosi hicho katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT (Mei 22, 2016) na fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) watakayokipiga na Yanga Mei 25 mwaka huu.

Makocha hao wanatarajia kurejea nchini Hispania mwishoni mwa wiki hii watakapomaliza kuishuhudia mechi ya Azam FC dhidi ya Mgambo JKT (Azam Complex), huko watakwenda kujipanga upya kwa ajili ya kuanza kukinoa kikosi hicho msimu ujao wakiwa wamekamilika wote kwenye benchi lao.

Changamoto ya kwanza kwa makocha hao itakuwa ni kukiongoza kikosi hicho kutetea ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame walioutwaa Agosti mwaka jana, safari hii michuano hiyo ikiendelea kusalia hapa nchini na itaanza rasmi Julai 16 hadi 30 mwaka huu.

Chanzo:azamfc.co.tz