KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo jioni imeingia mkataba na mabeki wawili, Mghana Daniel Amoah na Mzimbabwe, Bruce Kangwa, kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Wawili hao kila mmoja amesaini mkataba wa miaka mitatu, Amoah anayecheza beki ya kati ametokea Medeama ya Ghana, huku Kangwa aliyefuzu majaribio ya kujiunga na Azam FC akitokea kwa vinara wa Ligi Kuu Zimbabwe Highlanders.
Amoah, 18, anatua Azam FC ikiwa ni pendekezo la benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, ambaye alivutiwa naye kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika wakati akiichezea Medeama dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, huku yeye akifunga bao pekee la timu yake lililowapa sare ya bao 1-1.
Mbali na kuichezea Medeama, Amoah pia yupo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, ambacho kilitolewa na Senegal mwezi uliopita kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Zambia.
Mara baada ya kusaini mkataba huo, beki huyo kisiki anatarajia kuondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kurejea Ghana kwa ajili ya kuichezea mchezo wake wa mwisho timu yake hiyo dhidi ya TP Mazembe, ukiwa ni wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika leo Jumamosi, ambao una umuhimu mkubwa kwao kwani wapo kwenye nafasi nzuri ya kufuzu kwa nusu fainali ya michuano hiyo.
Mara baada ya mchezo huo utakaofanyika Agosti 14 mwaka huu, beki huyo atarejea nchini kwa ajili ya kuanza kazi rasmi ndani ya uzi wa Azam FC, ambayo mwakani itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Chanzo: www.azamfc.co.tz