Na dev.kisakuzi.com, Dar es Salaam
TIMU ya Mpira wa Miguu ya Azam FC ambao ni mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu Tanzania Bara, jana jijini Dar es Salaam ilimpelekea kombe la Ubingwa huo Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Azam inayomilikiwa na kampuni maarufu na tajiri Afrika Mashariki ya mfanyabiashara, Said Salim Bakhresa (SSB) inayotengeneza bidhaa mbalimbali nchini Tanzania ililazimika kulipeleka kombe hilo kwa Rais Kikwete baada ya rais kuvutiwa na kitendo cha Azam FC kuvunja historia ya miaka mingi ya kombe hilo kukaa mikononi mwa timu kubwa za jadi na zenye mashabiki na wapenzi wengi nchini Tanzania, yaani Simba na Yanga.
Rais Kikwete alivutiwa na hatua hiyo jana ndani ya Uwanja wa Uhuru baada ya kuwaona wafanyakazi wa kampuni ya SSB wakiwa kwenye maandamano ya maadhimisho ya kilele cha sherehe za siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi huku wakiwa wamebeba kombe hilo na kushangilia kwa sauti wakisema; ‘Bingwa, Bingwa, Bingwa’.
Baada ya wafanyakazi hao wa SSB kupita mbele ya Rais Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho hayo aliomba kombe hilo lipitishwe tena kwa mara nyingine ili atoe salaam zake na pongezi, kutokana na changamoto ambayo Azam FC imeionesha katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Wafanyakazi wa SSB walipita kwa mara ya pili na kulionesha kombe hilo kwa Rais Kikwete ambaye alisimama na kupunga mkono akiashiria salamu kisha kuruhusu wapite na kuendelea na shughuli nyingine. Azam FC walikuwa kivutio kikubwa katika maandamano ya Mei Mosi jana baada ya kulibeba kombe hilo la ubingwa wa bara kwenye gari la wazi na kushuhudiwa na wananchi wengine.
Katika msafara wa kombe hilo pia nyuma ulifuatiwa na basi maalumu la kisasa ambalo hutumiwa na wachezaji wa Azam FC wakiwa katika shughuli zao mbalimbali za kimichezo. Basi hilo la kisasa pia lilikuwa kivutio kingine kwa washiriki wa maadhimisho ya Mei Mosi kutokana na muonekano wake.