KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kujiandaa na kisayansi kuelekea mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam FC katika kujiandaa na michuano hiyo kisayansi, mwishoni mwa mwezi uliopita ilisafiri hadi jijini Ndola, Zambia kushiriki michuano maalumu ya timu nne na kutwaa ubingwa huo.
Safari hii Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, imepiga bao tena katika maandalizi yake baada ya kuzisoma kiufundi timu za Bidvest Wits ya Afrika Kusini na Light Stars ya Shelisheli, ambazo mojawapo itakutana na Azam FC katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.
Makocha wasaidizi wa Azam FC, Mario Marinica na Dennis Kitambi, walikuwepo nchini Shelisheli Jumamosi iliyopita kushuhudia mchezo wa raundi ya awali ya michuano hiyo, ambao Bidvest Wits walishinda mabao 3-0.
Mara baada ya kurejea kutoka kwenye kazi hiyo maalumu, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema wamefanikiwa kuwasoma wapinzani wao wote huku akidai kuwa Bidvest ilitumia zaidi kikosi cha wachezaji wengi vijana kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.
“Dhumuni letu kwenda kule tulikuwa tunataka kuwaona wapinzani wetu tutakaocheza nao katika raundi inayofuata, tulipokwenda kule tulikuwa tunajua ya kuwa tutakutana na Bidvest katika raundi ijayo kutokana na aina ya mpinzani waliokutana naye, lakini tulikuwa tunataka kuhakikisha tunawaona Light Stars namna wanavyocheza, kwani huwezi kujua lolote linaweza kutokea kwenye soka.
“Bidvest tulishawasoma kwenye mechi zao nyingi za Ligi Kuu Afrika Kusini na tunazo baadhi ya DVD zao, lakini tulichokiona kule ni wao walitumia kikosi cha vijana zaidi na ni tofauti na tulivyowaona katika mechi zao za ligi,” alisema Kitambi.
Kitambi alisema kwa sasa wanachoangalia zaidi ni kusafiri tena kuelekea Afrika Kusini kuwasoma tena Bidvest Wits katika moja ya mechi yao ligi, ili kuwasoma zaidi wapinzani wao hao wanaofundishwa na Gavin Hunt.
Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Azam FC ndio timu pekee ya Afrika Mashariki iliyoanzia raundi ya kwanza, ambapo itaanzia ugenini kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya moja ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kumalizia nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.
Habari na mantandao wa Azam FC.