KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameendelea kukiandaa kikosi chake kisayansi zaidi, ambapo amewashangaza baadhi ya wakazi wa Visiwani Zanzibar baada ya kuwafanyisha zoezi la kuendesha baiskeli barabarani wachezaji wake.
Kikosi cha Azam FC hivi sasa kinaendelea na mazoezi makali visiwani hapa ilipoweka kambi ya wiki moja, ambapo katika muendelezo wa mechi za kirafiki jana iliweza kuichapa Kombaini ya Wilaya ya Mjini bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji aliyeko kwenye majaribio Fuadi Ndayisenga.
Katika muendelezo wa programu zake kwenye kambi hiyo, jana saa 4 asubuhi Zeben aliwafanyisha zoezi la kuendesha baiskeli wachezaji wake, wakiendesha kwa takribani saa mbili wakianzia katika Hoteli ya Mtoni Marine walipofikia kuelekea Bububu hadi Amaan na kuitafuta tena njia ya kurejea hotelini walipoanzia.
Programu hiyo mpya kabisa kwa wachezaji ambayo haijazoeleka kufanywa na wachezaji wa timu yoyote hapa nchini, ilisimamiwa kwa ukaribu na Kocha Msaidizi wa Viungo wa Azam FC, Pablo Borges.
Licha ya ugumu wa programu hiyo ya kuendesha baiskeli umbali mrefu pamoja na kupanda vilima vitatu tofauti pamoja na mvua iliyokuwa ikinyesha kwa nyakati tofauti, wachezaji walionekana kufurahia mazoezi hayo, ambayo ni mahususi kwa kujenga nguvu za miguu, pumzi na kasi.
Cha kufurahisha zaidi kila eneo walilopita watu walionekana kushangaa wakidhania ni mashindano ya baiskeli, lakini baadaye walikuja kugundua ni mazoezi tu ya wachezaji wa Azam FC na kubakia kuwashangilia na kuwapungia mikono kila walipopita.
Wakati huo huo timu hiyo jana ilitimiza miaka nane tokea ipande rasmi Ligi Kuu mwaka 2008 tarehe kama ya jana (Julai 27), ambapo ilipanda baada ya kuichapa Majimaji ya Songea mabao 2-0, mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Chanzo: azamfc.co.tz