Na Anna Nkinda – Maelezo, Washington
CHAMA cha Wanawake wa Afrika na Uelewa wa Saratani (African Women Cancer Awareness Assossiation – AWCAA) imemkabidhi Mke wa Rais Mama Salma Kikwete mashine moja inayotumika kupima ugonjwa wa saratani ya matiti yenye thamani yazaidi dola za kimarekani laki mbili.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini Washington D.C nchini Marekani. Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mashine hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alikishukuru chama hicho kwa mashine waliyowapatia wanawake wa Tanzania na kusema itaokoa maisha ya wanawake wengi. Alisema ugonjwa wa saratani ya wanawake ambazo ni matiti na shingo ya kizazi zinaua wanawake wengi lakini wengi zaidi wanakufa kwa saratani ya shingo ya kizazi ukilinganisha na magonjwa mengine kama maralia na Ukimwi
Mama Kikwete alisema, “Tunaishukuru Serikali yetu kwa jitihada inazozifanya dhidi ya ugonjwa huu, lakini bado utambuzi wa ugonjwa ni mdogo kwani bado kuna tatizo la unyanyapaa miongoni mwa jamii jambo linalosababisha wanawake wenye matatizo kuogopa kusema na hivyo kutambuliwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa ambayo haina njia mbadala”.
Alisema WAMA kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) wanafanya kazi ya kuwaelimisha wananchi ili waweze kuutambua ugonjwa huo na wanawake wameelekezwa jinsi ya kujipima wenyewe saratani ya matiti.
Pia madaktari kupitia kampeni maalum wanaenda mikoani kuwapima wanawake ambao wakikutwa na matatizo wanaandikiwa na kwenda kupata matibabu katika Hospitali za Rufaa za Kilimanjaro, Mbeya na Bugando.
Mama Kikwete alisema; “Tatizo lililopo mashine za Mammogram ni chache, wanawake wengi wanaoishi vijijini hawawezi kusafiri na kwenda kupata huduma za matibabu kutokana na ukosefu wa nauli lakini wakati wa kampeni za upimaji wanajitikeza kwa wingi. Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha mashine zinapatikana kwa wingi pia jamii ikiondoa unyanyapaa kila kitu kitawezekana kwani hivi sasa teknolojia imekuwa mtu anatibiwa na kupona saratani hafi kama ilivyokuwa zamani”.
Akiongea mara baada ya kukabidhi mashine hiyo Mwanzilishi wa AWCAA Mama Ify Nwanbuku alisema wanawake wengi wa Afrika wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa wa saratani kwa vile hawana uelewa kuhusu ugonjwa huo na pia upatikanaji wa huduma za matibabu ni mgumu.
Alisema kazi wanazozifanya ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani ya matiti, kusaidia wanawake takriban 100 kwa mwaka ili waweze kufanyiwa uchunguzi na kupata huduma ya saratani ya matiti, kutoa huduma za kijamii kwa wagonjwa zikiwemo za kifedha na misaada na kutoa misaada kwa watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki kwa saratani.
“Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya wa nchini Marekani tunafanya kazi hizi ndani ya Marekani kwa kuwasaidia wanawake wenzetu wa kiafrika na pia katika nchi za Afrika tunafanya kazi katika nchi za Sudani, Cameroon, Nigeria na ninaamini siku moja tutakuja kufanya kazi nchini Tanzania ili tuweze kuwasaidia na wenzetu wa huko,” alisema Nwanbuku.
Kwa upande wake Asha Hariz ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake wajasiriamali wa Tanzania waishio nchini Marekani cha Wanawake watano (Tano Ladies) ambao ndiyo walisaidia kupatikana kwa mashine hiyo alisema wanaamini mashine ya Mammogram itasaidia kuokoa maisha ya wanawake nchini Tanzania ambayo ni moja ya malengo ya WAMA.
Alisema nchini Marekani kuna watu milioni mbili na laki tisa wanaishi na saratani hii ni baada ya kujikinga mapema, kupata elimu ya saratani ya matiti na kufanyiwa uchunguzi hivyo basi hata nchini Tanzania kama wanawake wenye saratani watagundulika mapema na kupata matibabu wataweza kuishi muda mrefu.
Hariz alisema, “Tunaelewa kwamba mgonjwa akipata huduma na kujikinga mapema hatakufa kwa sababu katika jamii yetu kuna watu wanaoishi na saratani ya matiti kwa muda mrefu ambao hivi sasa wanafanya kazi ya kuilelimisha jamii ili watu waweze kupima na kuufahamu ugonjwa huu.”
Chama cha Wanawake wa Afrika na Uelewa wa Saratani kilianzishwa mwaka 2004 kwa kushirikiana na wanawake wa kiafrika wahamiaji na wataalamu wa afya kwa ajili ya kuondoa utofauti katika uelewa, kujikinga na kupata huduma za Afra kwa jamii ya waafrika wahamiaji wanaopata ugonjwa wa kansa. Kikundi hicho kimekuwa na kuongeza wataalamu wa afya, wajasiriamali na watu wanaoguswa na malengo ya kikundi ya kutoa tofauti ndani ya wakazi wa Washington, Bara la Afrika na Duniani kote.