AU Yaipongeza APRM kwa Kuchagiza Maendeleo ya Afrika

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma

Na Hassan Abbas, Addis Ababa

UMOJA wa Afrika umeupongeza Mpango wake wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) kwa kuzisaidia nchi za Afrika kuepuka migogoro, kuweka msiingi imara ya maendeleo na kujenga demokrasia ya pamoja.

Kauli hiyo imetolewa mjini hapa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma alipokuwa akishiriki katika mjadala wa viongozi kuhusu mchango wa vyombo vya habari vya Afrika katika maendeleo ya Bara hilo.

“APRM ni Mpango muhimu sana katika kuboresha demokrasia barani Afrika na ndio maana nchi nyingi zaidi zinazidi kujiunga. Mwanzoni zilikuwa ni nchi chache lakini sasa kuna takribani nchi 32 zinazoshiriki,” alisema.

Alisisitiza kuwa APRM inasaidia Serikali na watu wake kukubaliana kwa pamoja ni masuala gani yanawakwaza kimaendeleo na kisiasa wao kama Taifa ili yafanyiwekazi na maeneo gani Taifa linafanya vyema ili kuendelea kuenzi neema hiyo.

“Katika APRM lengo si kukosoana wala kutafuta mchawi. Huu ni Mpango wetu madhubuti ambapo nchi inajiunga kwa hiari kisha inashirikisha wadau wake wakiwemo wananchi, vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali kusema jamani hapa tuko vizuri na pale tunahitaji jitihada za pamoja kuboresha,” alisema mama Zuma.

Kauli hiyo juu ya umuhimu wa APRM inakuja ikiwa ni siku chache tu tangu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon naye kuueleza Mpango huo kama “chache ya kuboresha demokrasia Afrika,” na kutaka uimarishwe zaidi alipozungumza mjini New York wakati wa Wiki ya Afrika mwezi uliopita.

Akizungumzia umuhimu wa APRM katika kutatua migogoro, Dr. Nkosazana alitoa mfano wa Ripoti ya APRM nchini Kenya ambayo mwaka 2007 kabla ya uchaguzi ilishauri masuala kadha kuhusu umuhimu wa kuwa na Katiba mpya kabla ya uchaguzi na kugusia viashiria vingine.

“Wenzetu Kenya wakati huo wakapuuzia ushauri huo wa APRM na tukaona nchi ikaingia katika machafuko. Kwa hiyo APRM kwa upande mmoja inasaidia kuonesha viashiria vya mitafaruku na kushauri vifanyiwe kazi mapema,” alisema mbele ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto aliyehudhuria pia mkutano huo.

Dr. Nkosazana alitumia fursa hiyo kueleza changamoto zinazoikabili APRM kwa sasa ni kuongezeka kwa nchi zinazoomba kufanyiwa tathmini wakati ambapo uwezo wa sasa wa kitaasisi kufanya tathmini ni nchi mbili tu kwa mwaka. Akasisitiza kuimarishwa uwezo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizojiunga mwanzoni tu mwaka 2004 tangu APRM ilipoanzishwa rasmi Machi, 2004. Hivi sasa Tanzania imeshafanyiwa tathmini na hivi karibuni itaizindua Ripoti yake ya Hali ya Utawala Bora iliyosheheni maoni ya wananchi na wataalamu na umeandaliwa pia Mpango wa Utekelezaji.