Na Mwandishi Maalumu, Ghana
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Ijumaa, Agosti 10, 2012, amekuwa miongoni mwa viongozi mbali mbali duniani walioshiriki katika shughuli za mazishi ya aliyekuwa Rais wa Ghana, Profesa John Evans Atta Mills, ambaye amezikwa kwenye bustani ya Geese Park, Marine Drive, mjini Accra.
Mwili wa Rais Mills uliteremshwa kaburini saa 11 na dakika 25 jioni baada ya shughuli za mazishi ikiwamo ibada ya mazishi iliyoendeshwa na mchanganyiko wa dini na madhehebu yote makubwa katika Ghana zilizofanyika kwenye Independence Square mjini Accra na kuchukua kiasi cha saa saba kuanzia saa nne asubuhi.
Rais John Evans Atta Mills alifariki dunia saa nane na robo mchana wa Julai 24, mwaka huu, 2012 siku tatu tu baada ya kuwa amesheherekea miaka 68 ya kuzaliwa kwake.
Kabla ya kushiriki katika shughuli za mazishi za kiongozi huyo wa Ghana ambaye aliapishwa kuongoza taifa hili la Afrika Magharibi
Januari 7, 2009, Rais Kikwete na marais na viongozi wengine alitia
saini kitabu cha maombolezo katika shughuli iliyofanyika kwenye jengo la Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Accra (AICC) lililoko jirani na Independence square.
Mbali na Rais Kikwete na rais mwenyeji John Dramani Mahama, mazishi hayo yamehudhuriwa na marais kutoka Liberia, Benin, Togo, Burkina Faso, Nigeria, Ivory Coast na Niger. Mazishi pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wane, maspika wa mabunge manne na wawakilishi wa nchi 53 duniani akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton. Miongoni mwa wazungumzaji wakubwa kwenye shughuli hiyo walikuwa ni pamoja na Rais Mahama, mtoto wa marehemu Rais Mills, Kofi Sam Atta Mills na mjane wa marehemu Dr. Ernestina Atta Mills na mdogo wake marehemu, Dr. Cadman Atta Mills.