MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani ameteuliwa kuwemo kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo wa CAF kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu una jumla ya watu 148.
Nyamlani ni mmoja wa wajumbe watatu watakaoshughulikia masuala ya rufani. Wajumbe wengine ni Prosper Abega kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon. Nyamlani ni mjumbe wa Bodi ya Rufani ya CAF yenye watu 12.
Wakati huo huo, Mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville iliyochezwa juzi (Novemba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,021,000.
Mapato hayo yametokana na washabiki 18,022 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 10,000, sh. 5,000, sh. 2,000 na sh. 1,000. Washabiki 15,850 walikata tiketi za sh. 1,000.
Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 3,511,677.97 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 5,956,635), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh. 400,000), Wachina- Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na ulinzi wa mechi (sh. 3,500,000).
Kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 1,000,537, asilimia 10 ya uwanja sh. 500,269, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 250,134, asilimia 45 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,251,209, asilimia 20 ya TFF (sh. 1,000,537) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 50,027.