MWENYEKITI wa mtaa wa Centrol Tanga, Diana Mussa, amewataka wakazi wa eneo hilo kuweka mazingira ya usafi kwa kila nyumba ili kuondosha kitisho cha magonjwa ya milipuko na kusema kuwa ambaye atakaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria. Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa duka la kuuza umeme la Zola lililopo barabara ya Markert Street Tanga juzi , Diana amesema agizo hilo litakuwa endelevu na ofisi yake ikiongozwa na yeye kila siku asubuhi atafanya ukaguzi kwa kila mtaa.
Amesema halmashauri ya jiji imeweka vyombo maalumu vya kuhifadhia takataka na magari ya kusomba taka mtaani hivyo kutaka kila mmoja kuhakikisha eneo lake linakuwa katika mazingira mazuri.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Meneja mauzo kanda ya Kaskazini Tanga na Kilimanjaro, Peter Laizer, amewataka wajasiriamali wadogowadogo kutumia umeme wa Zola na kusema kuwa ni wa gharama nafuu.
Amesema Wajasiriamali wa mbogamboga na matunda wanaweza kuinua kipato chao kwa kusindika na kuweza kusafirisha kwenda katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako watajitangaza tofauti na kutegemea mteja mmoja mmoja.
Amesema umeme huo ni mkombozi kwa watu wa kipato chote, cha chini, kati na juu na, umeme huo utaondolea adha mbalimbali kama za kuchaji simu mbali na nyumbani na ufuatiliaji wa taarifa katika Luninga pamoja na kusaidia watoto kusoma katika mwanga bora nyakati za usiku.
“Umeme huu ni mkombozi kwa wananchi wa Tanga kwani ni rahisi, hauchukui muda kuupata na pia utawasaidia wananchi kuhifadhi kiasi cha pesa ambacho walikuwa wanakitumia kwa nishati nyingine kupata mwanga, Pia humsaidia mwananchi wa kipato cha chini kubadilisha maisha kwa kupata habari, taarifa pamoja na burudani, kwani mbali na taa na kuchaji simu pia utapata Radio na TV za sola”alisema Laizer
Alisema umeme huo umekuwa mkombozi kwa wanafunzi wa vijijini ambao walikuwa hawana uwezo wa kujisomea usiku au husoma katika mwanga hafifu wa vibatari sasa wanapata mwanga salama kwa afya ya mwili na macho.