Askofu Kilaini Afiwa na Baba Yake, Ikulu Yatoa Pole…!

Askofu Methodius Kilaini akiwa kazini

Askofu Methodius Kilaini akiwa kazini


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Askofu Methodius Kilaini, akimpa pole kwa kifo cha baba yake mzazi, Mzee Paulo Mutegeki Kilaini.

Katika salamu hizo zilizotumwa leo, Aprili 4, 2014, Rais Kikwete amemwambia Askofu Kilaini: “Kwa masikitiko makubwa, nakupa pole nyingi na naungana nawe katika kuomboleza kifo cha Baba yetu, Mzee Paulo Kilaini, ambacho nimejulishwa kuwa kilitokea asubuhi ya jana katika Hospitali ya Mbweni, Dar Es Salaam.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Mzee Kilaini alikuwa mpenda maendeleo na siku zote alikuwa mstari wa mbele katika kusaka maendeleo ya jamii yake na hasa hasa atakumbukwa kwa juhudi zake kubwa katika maendeleo ya elimu. Aidha, ni dhahiri kuwa Mzee Kilaini ametuacha wakati busara zake zikiwa zinahitajika zaidi katika jamii yetu”.

Amesisitiza Mhe. Rais: “Baba Askofu, najua kuwa kwako wewe na familia nzima ya Mzee Paulo Mutegeki Kilaini hiki ni kipindi kigumu. Hivyo, nawatakieni rehema za Mwenyezi Mungu, awape uvumilivu na subira huko mkielewa kuwa niko nanyi wakati wote wa msiba kwa sababu msiba huu pia ni msiba wangu. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Mzee Paulo Mutegeki Kilaini. Amina.”