Askari KINAPA walalamikiwa

Sehemu ya hifadhi ya mlima Kilimanjaro inayomilikiwa na KINAPA


Na mwandishi wetu
Moshi.

WANANCHI wa kijiji cha Sungu kata ya Kibosho mashariki wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamewalalamikia askari wa hifadhi ya Kilimanjaro (KINAPA) kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo, na badala yake kujiingiza kwenye vitendo vya uvunaji miti na kupasua mbao, katika msitu unaozunguka hifadhi hiyo.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho, wananchi hao walisema wapo baadhi ya askari wa hifadhi ya kinapa, ambao wamekuwa hawafanyi kazi na badala yake kufanya biashara ya mbao.

Walisema askari hao ambao wamepewa kazi ya ulinzi katika hifadhi hiyo, wamekuwa wakiingia msituni na kufanya biashara ya kuuza magogo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,huku wakiwazuia wananchi wanaoishi maeneo ya kuzunguka msitu huo kuingia msituni kwa ajili ya kukata majani ya mifugo.

“Kuna askari wa kinapa ambao wamekuwa hawaji msituni kwa ajili ya kulinda bali kufanya biashara,askari hawa wamekuwa wakija msituni na kuuza magogo lakini wananchi wamekuwa wakizuiwa kuingia msituni kwa ajili ya kukata majani na hata wakiingia askari hao huwatesa sana na kuwafukuza”alisema Vendeline mmoja wa wananchi hao.

Wananchi hao walisema jambo ambalo limekuwa likiwashangaza na kuwaumiza ni kuona mbao zikiendelea kupasuliwa ndani ya msitu huku askari wakiwepo jambo ambalo ni kinyume cha sheria na serikali mkoani humo imeshapiga usauaji mbao na utoaji wa vibali vya uvunaji miti.

Walisema wakati vitendo hivyo vikiendelea, walijaribu kuwasiliana na afisa maliasili wilaya bila mafanikio hali ambayo waliiomba serikali ya mkoa kuangalia uwezekano wa kushirikisha mgambo wa kata katika suala la ulinzi wa msitu ili kuweza kuwadhibiti wa vamizi wa uharibifu wa mazingira, pamoja na askari wa hifadhi ambao si waaminifu.

Aidha afisa maliasili wilaya ya Moshi Msami Mshana alipoulizwa na mkuu wa mkoa kuhusiana na malalamiko ya wananchi,alikiri kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusiana na uvunaji wa miti katika msitu lakini hakuweza kufika kutokana na kwamba alikuwa likizo.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa Leonidas Gama alitoa wiki mbili kwa ofisa huyo wa maliasili, kuhakikisha anakutana na uongozi wa Kinapa ili kufika katika kijiji hicho kusikiliza malalamiko ya wananchi, na kuyashughulikia mara moja.

“Nakuagiza afisa maliasili ndani ya wiki mbili upate majibu ya matatizo haya ya wananchi,kama wananchi wanateseka na kuonewa, na askari wa Kinapa wanafanya biashara ndani ya msitu, naomba nipate majibu hayo ndani ya wiki mbili, kwani kama tumezuia miti kukatwa kanini hapa inakatwa”alisema Gama.