Na Mwandishi Wetu–Maelezo
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi amesema askari anayetuhumiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel 10, marehemu Daudi Mwangosi amefikishwa mahakamani leo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo iliyosainiwa na Waziri Nchimbi ilieleza kwamba Septemba 7, mwaka huu alikabidhiwa taarifa ya awali ya uchunguzi wa polisi juu ya kifo cha mwandishi huyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema.
Hivyo Septemba 11, mwaka huu aliliagiza Jeshi la Polisi kumpeleka mtuhumiwa huyo askari namba G. 2573 PC Pasifious mahakamani leo kama ilivyotakiwa ma Mkurugenzi wa Mshtaka (DPP).
Waziri Nchimbi alisema wakati mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani, kamati iliyoundwa chini ya Jaji Ihema itaendelea na kazi yake ili kupata suluhisho la kudumu la migongano ya kikazi kati ya polisi na waandishi wa habari na waandishi wa habari, polisi na vyama vya siasa ikiwemo kuboresha mahusiano zaidi kati ya polisi na raia. Aliongeza kuwa mkondo wa sheria umeanza kufuatwa nawaomba wadau wote kutoa nafasi kwa utaratibu huo wa kisheria kufanya kazi.
Aidha aliongeza kuwa uchunguzi huo wa awali ulibaini mambo makubwa mawili, ambayo ni mlipuko uliotokea ulitokana na bomu la Machozi na bomu hilo lilifyatuliwa na askari huyo. Kwa mujibu wa taratibu za Jeshi la Polisi tayari askari huyo amefukuzwa kazi mara baada ya kupanda kizimbani.
WAKATI huo huo: Mtandao wa francisgodwin.blogspot.com unaripoti kuwa mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten Daud Mwangosi leo amefikishwa mahakamani. Mtuhumiwa huyo amefikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi ya Wilaya kujibu shitaka lilalomkabili.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa serikali Mkuu Michael Luena, amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni askari mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23) mkazi wa FFU Iringa, anakabiliwa na shitakala la mauaji ya makusudi.
Amesema mtuhumiwa huyo mnamo Septemba 02mwaka huu katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa alimuua Daudi Mwangosi kwa makusudi kinyume na kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo 5A.i cha makosa ya jinai.
Mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa mahakama ya hakimu Mfawidhi ya Wilaya Dyness Lyimo mtuhumumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haiwezi kusikiliza kesi za mauaji. Kwa mujibu wa kesi za jinai, sheria kifungu 196 kanuni ya adhabu Cap. 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, kinakataza mtuhumiwa wa mauaji ya kukusudia kupewa dhamana. Mtuhumiwa amerudishwa mahabusu kutokana na kesi yake kukosa dhamana kisheria na kesi hiyo imeahirishwa hadi 26 Septemba mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Hata hivyo askari wengi waliompeleka mtuhumiwa huyo wakiwa wamevaa nguo za kiraia walihakikisha kuwa mtuhumiwa huyo hapigwi picha jambalo limewaletea ugumu waandishi waliokuwapo baada ya kusukumwa ovyo kuzuia mtuhumiwa huyo asipigwe picha. Kila wakati waandishi walipotaka kupika picha walikuwa wakisukumwa na askari hao huku mtuhumiwa akiwa amejifunika kichwa na kuziba uso kuhakikisha kuwa sura yake haionekanai na waandishi hao.
Katika hali isiyo ya kawaida mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani hapo kwa gari binafsi la kifahari lenye namba za usajili T 320 ARC Toyota Land cruiser GX tofauti na watuhumiwa wengine ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa gari la polisi.