Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Sheria na Katiba Tanzania, Celina Kombani amesema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizoendeshwa zimebaini kuwa asilimia 44 ya wanawake nchini wamekutana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa waume zao.
Kombani ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua kampeni ya kupinga Unyanyasaji wa Kijinsia. Pamoja na hayo Kombani amesema vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa si Tanzania pekee bali hata mataifa mengine, huku akieleza kwamba tatizo hilo linachangiwa na mila potofu na umasikini.
Hata hivyo, Waziri Kombani amesema kumekuwa na dhana potofu kuwa unyanyasaji hufanyika kwa wanawake tu, lakini ukweli ni kwamba hata wanaume hukumbwa na unyanyasaji huo kutoka kwa wake zao.
Kutokana na hali hiyo Waziri Kombani ametoa wito kwa wanawake wenye tabia hizo kuacha mara moja ambapo amewataka wanandoa kuishi kwa upendo ili kujenga familia sikivu na bora.
Kampeni za kupinga unyanyasaji wa kijinsia zimefanikiwa kwa kushirikiana na Mradi wa Champion unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto.