MKURUGENZI wa Kampuni ya The African Stars Entertainment (ASET), Asha Baraka, ameanzisha taasisi ya kuvumbua vipaji itakayojulikana kwa jina la Twanga Academia.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, amesema kwamba, Twanga Academia tayari imenunua vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 100 kwa ajili ya kuanzia katika taasisi hiyo.
Amesema ili kupata vijana wa kuanza mafunzo hayo ya muziki wa dance, wamepanga kufanya usaili wa kusaka vipaji mbalimbali vya muziki huo, Jumapili ijayo kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 6:00 mchana.
Asha aliongeza kuwa, usaili huo, utasimamiwa na magwiji wa muziki wa dansi, kama Hamza Kalala ‘Komandoo au Mzee wa Madongo’, Rais wa FM Academia, Nyoshi El Saadat na wengineo kadhaa, ambako watatoa fursa kwa chipukizi wanye uwezo wa kutumia ala za muziki.
“Lengo la Twanga Academia, ni kusaka vipaji vya waimbaji, pamoja na wanamuziki wenye uwezo wa kupiga ala, ambavyo vitaendelezwa kwa kupitia wakufunzi watakaowafunda mara baada ya kupatikana,” alisema Asha.
Kwa upande wake, Mkongwe Komandoo Kalala, alimpongeza Asha kwa hatua hiyo aliyofikia na kwamba, ndiye atakuwa wa kwanza kukumbuka kuvumbua vipaji vya wapigaji wa ala za muziki.
“Hiki kitu mimi nilikuwa nakizungumzia kila siku, kwani ni wanamuziki wachache sana, ambao wanajua kuimba na kutumia ala, wengi ni washika vipaza sauti tu, mambo mengine hawajui, lakini hawajachelewa wanaweza kuanza sasa, kwani elimu haina mwisho,” alisema Kalala.
Aliongeza kuwa, binafsi anamuunga mkono Asha, kutokana na kuja na wazo hilo jipya.
“Tunaliheshimu wazo lake jipya alilokuja nalo na tutaitumia nafasi hiyo, kwa kuwapa elimu wanamuziki chipukizi ili kuongeza tija kwa wapiga ala, tofauti na ilivyo hivi sasa,” alisema.
Alitoa wito kwa wazazi na walezi, kuwapa ruhusa vijana wao kwenda katika usaili siku hiyo itakapofika. Mbali ya kusaka wanamuziki watakaomudu kupiga ala, pia watakaojitokeza watafundishwa kuimba na kucheza, ambako zoezi hilo pia linawahusu wasanii wa mikoani hivyo wajitokeze.