ARSENE Wenger amesema alitaabika sana wakati wa msimu huu wa usajili na kuuelezea kuwa ni “usajili ulionisumbua ambao haujawahi kutokea tangu niwasili hapa”.
Gunners ilimuuza Cesc Fabregas, Samir Nasri na Gael Clichy kwa klabu za Barcelona na Manchester City na wameuanza msimu huu vibaya sana, wakadhalilishwa kwa kubugizwa mabao 8-2 na Manchester United.
Meneja huyo wa Arsenal amesema: “Katika kazi yangu, unatazamia kupata shida kubwa. “Ndio maana siku moja nilisema potelea mbali, ni maumivu madogo kwangu kuliko kwako, kwa sababu nimezoea kuumia.”
Wenger ameongeza kusema: “Ninaweza kuandika kitabu kuhusiana na msimu huu wa usajili. Kitabu hicho kitakuwa kizuri kukisoma. “Si kwa sababu ni mimi niliyeandika, lakini ni kutokana na yote yaliyotokea. Huwezi kuamini.”
Wakati huohuo, Wenger anatumai kiungo mshambuliaji mpya Mikel Arteta kuanza kuonesha “cheche zake mara moja” dhdi ya Swansea siku ya Jumamosi. Mbali na Arteta wachezaji wengine waliosajiliwa msimu huu wanaweza kucheza akiwemo Per Mertesacker, Yossi Benayoun, Andre Santos na Chu Young Park.
Wenger amesema: “Kwetu, ni mwanzo mzuri. Natumai Arteta ataonesha cheche haraka pamoja na Benayoun. “Ni wachezaji wanaonivutia kutokana na uhodari wao kiufundi.”
Wenger ana matumaini mtindo wa uchezaji wa timu hiyo utawavutia pia wachezaji hao wapya. Amesema: “Ni wachezaji wanaojua kuutumia uwanja na wana kipaji. Huo ndio mchezo tunaotaka kuucheza kwa hiyo watauzoea vizuri na haraka.