Matumaini ya Arsenal kutwaa taji la ligi ya Uingereza kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12 yalipata pigo baada yao kulazwa 2-1 na Swansea uwanjani Emirates.
Arsenal walikuwa wakiongoza, kupitia bao la Joel Campell na ilionekana kana kwamba wangepunguza mwanya kati yao na viongozi Leicester.
Lakini Swansea, waliokuwa bila meneja wao Francesco Guidolin, walisawazisha kupitia Wayne Routledge.
Olivier Giroud na Alexis Sanchez waligonga mwamba wa goli lakini bahati haikusimama.
Ashley Williams aliwaadhibu na kufungia Swansea bao la ushindi na mwishowe Arsenal wakalazimishiwa kichapo cha 2-1.
Arsenal sasa wamo alama sita nyuma ya viongozi wa ligi Leicester City.
Tottenham, ambao walikuwa na fursa ya kwenda kileleni, nao pia waliteleza baada ya kuchezewa vilivyo na West Ham uwanjani Upton Park na kupewa kipigo cha 1-0.
Bao hilo lilifungwa kwa kichwa na Michail Antonio dakika ya saba.
Uwanjani Anfield, Liverpool walilipiza kisasi kushindwa na Manchester City kwenye Kombe la Ligi kwa kuichapa klabu hiyo ya Etihad 3-0.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Adam Lallana, James Milner na Roberto Firmino.
Uwanjani Old Trafford, Manchester United walikwepa msiba wa miamba wa ligi kwa kuandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Watford. Bao la United lilifungwa na Juan Mata.
Matokeo kamili ya mechi zilizochezwa Jumatano usiku:
• Arsenal 1-2 Swansea
• Stoke 1-0 Newcastle
• West Ham 1-0 Tottenham
• Liverpool 3-0 Man City
• Man Utd 1-0 Watford