APRM Yawasilisha Maoni ya Katiba Mpya

Hayo yalielezwajijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alipokuwa akiwasilisha maoni ya taasisi hiyo mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania umeshauri kuwa ni vyema suala la muundo gani wa Muungano unafaa likaachiwa wananchi kuamua ili kuijenga jamii bora ijayo.
Hayo yalielezwa juzi (Jumatano) jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alipokuwa akiwasilisha maoni ya taasisi hiyo mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akifafanua hilo, Bi Rehema alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na APRM kuhusu hali ya utawala bora nchini ingawa kero za Muungano zinajulikana maoni ya wananchi yamegawanyika sana kuhusu ni Muungano gani unaofaa zaidi.
“Wadau wa APRM wanapendekeza kwamba kwa kuwa suala hili linahusu mustakabali wa nchi na kwa kuwa Katiba ya sasa inasema mamlaka yote yako kwa wananchi-Muundo na kero nyingine za Muungano viamuliwe kwa kuzingatia maoni ya wananchi wenyewe yanayohusu namna bora zaidi ya kuuboresha,” alisema Bi Rehema.
Bi Twalib pia alisema ni maoni ya APRM kuwa Tume ya Mrekebisho ya Katiba inajukumu zito kuhakikisha kuwa mchakato wa mabadiliko ya katiba unakuwa wa wazi na shirikishi ili kuwapa Watanzania fursa ya kukata kiu yao ya muda mrefu ya kuwa na katiba mpya.
“Tanzania ni moja ya nchi zenye amani na demokrasia iliyotukuka kutokana na misingi imara ya kiuongozi iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere. Hata hivyo katika harakati za ujenzi wa Taifa imara la Tanzania zimekumbana na changamoto nyingi hasa baada ya kuingia katika mfumo wa nyama vingi.
“Wadau katika APRM wamemependekeza na wanaunga mkono mchakato wa kutungwa katiba mpya. Hata hivyo wameshauri mchakato wa kupata katiba mpya uchukuliwe kwa uzito wote kuwa ni fursa nyingine adhimu kuitengeneza Tanzania bora ijayo,” alisema.
Naye Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania aliieleza Tume hiyo kuwa katika eneo la uhuru wa habari ni vyema uandishi wa ibara zinazoainisha uhuru huo pia pamoja na utafiti mwingine ukazingatia maoni ya Mtaalamu-Elekezi wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu namna ya kuweka uwiano bora kati ya haki na wajibu wa vyombo vya habari.