Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MPANGO wa Bara la Africa Kujithmini Kiutawala Bora (APRM) Agosti 10 mwaka huu unatarajia kuzindua ripoti mpya itakayoonesha Hali ya Utawala Bora nchini kwa mujibu wa maoni ya wananchi na wataalamu mbalimbali.
Hayo yamesemwa mjini Dodoma na Afisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari na wananchi wa aina mbalimbali kwenye Maonesho ya Wakulima yanayoendelea ya Nane Nane kwenye viwanja vya Nzuguni.
“Ripoti hiyo imehuisha ile ya awali ya mwaka 2009 kwa nia ya kungeza takwimu kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyokwishajitokeza katika kipindi cha Julai mwaka huo hadi sasa,” alisema na kuongeza kuwa uzinduzi huo pia utawapa fursa wadau mbalimbali wa masuala ya utawala bora kuihakiki ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa Bw. Abbas wadau wapatao 100 wa masuala ya utawala bora watashiriki katika semina ya uzinduzi huo ambapo watafiti walioshiriki kuihuisha ripoti hiyo wataeleza mambo yaliyobainika katika utafiti wao wa hali ya utawala bora nchini na wadau watapata fursa ya kutoa maoni yao ili kuiboresha ripoti hiyo zaidi.
Aliongeza kuwa utafiti wa APRM umehusisha wataalamu hao kuangalia maeneo makuu manne ambayo ni demokrasia na utawala bora katika siasa; utawala bora katika mashirika ya umma; utawala bora katika uendeshaji wa makampuni na mwisho wamepitia namna nchi inavyowajibika katika utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
Akieleza chimbuko la APRM alisema kuwa ni mpango endelevu uliobuniwa na marais wa Afrika katika kikao chao cha mwaka 2002 ambapo walikubaliana kuweka utaratibu wa kila nchi kuanzisha taasisi hiyo na kisha kuipa jukumu la kufanyakazi ya kujitathmini mara kwa mara katika nyanja za utawala bora. Mkataba huo wa Afrika unaonesha kuwa nchi hutathminiwa kila baada ya miaka minne.
Taarifa zinaoneshan kuwa tayari nchi kadhaa za Afrika za Kenya, Rwanda na Ghana, zilikwishafanya hivyo na sasa zinarudia tena utafiti huo kwa mara ya pili ili kubaini changamoto mpya na kuzifanyikakazi.