APRM kueleza mafanikio, changamoto za utawala bora Zanzibar

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Amir Kificho

Na Hassan Abbas

MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) utawaeleza viongozi mbalimbali wa kisiasa na watendaji wengine Zanzibar juu ya mafanikio katika kujenga misingi ya utawala bora nchini katika miaka 50 ya uhuru na changmoto zake.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib mpango huo umeandaa semina mbili kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Makatibu Wakuu wa Wizara kwa lengo la kuwafahamisha kuhusu maoni ya wananchi kuhusu utawala bora nchini.

“Oktoba 18 mwaka huu tunatarajia kukutana na Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali na kisha Oktoba 23 kutakuwa na semina maalum kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,” alisema.

Kwa mujibu wa ripoti iliyohuishwa hivi karibuni ya APRM Tanzania, Tanzania kwa ujumla imeonekana kupiga hatua kubwa katika kuboresha misingi ya kisera na kisheria katika kukuza utawala bora nchini, ushiriki wa umma katika masuala ya uongozi na utawala umeimarika na nguvu za mihimili ya dola katika kuhakikisha nchi inakuwa imara zimeimarishwa.

Hata hivyo ripoti hiyo imeonesha kuwa wananchi na wataalamu mbalimbali waliohojiwa wameshauri kushughulikiwa changamoto anuai zikiwemo kero za Muungano, tatizo la uchumi mpana kutowafikia wananchi wengi na suala la katiba mpya.

APRM ni taasisi iliyobuniwa na viongozi wa nchi za Afrika (AU) mwanzoni mwa miaka ya 2000 kwa lengo la kuwashirikisha wananchi kuainisha mazuri ya utawala bora katika nchi zao ili yaimarishwe zaidi na pia kutaja changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 kati ya 54 za Afrika zilizoridhia mkataba wa kuanzishwa mpango wa APRM na hapa nchini taasisi hii iko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Ripoti za APRM kutoka kila nchi mwanachama mbali ya kuwasilishwa mbele ya wakuu wa nchi zinazoshiriki mpango huo kwa ajili ya kupeana uzoezi na kushauriana pia huandaliwa mpangokazi wa kitaifa wa miaka mitatu mitatu kwa ajili ya Serikali husika kufanyiakazi changamoto zilizobainishwa. Kwa mujibu wa mkataba, utafiti huu hurudiwa kila baada ya miaka minne.