Prof Adebeyo Olukoshi
Na Mwandishi Wetu MARAIS wa nchi za Afrika zinazoshiriki katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wamemteua Prof Adebeyo Olukoshi rais wa Nigeria kuwa Mtendaji Mkuu wa Mpango huo kwenye makao makuu yake yaliyoko Midrand, Afrika Kusini. Kabla ya uteuzi wake Prof. Olukoshi alikuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Umoja wa Mataifa cha Maendeleo ya Uchumi (UN African Institute for Economic Development and Planning, IDEP). Kitaaluma ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa kiuchumi na alipata pia kuwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Utafiti wa Sayansi Jamii (CODESRIA). Uteuzi huo unakuja ikiwa ni baada ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu, Assefa Sifa raia wa Ethiopia kumaliza muda wake na nafasi hiyo kushikwa kwa kipindi cha mpito na Mtendaji Mkuu wa NEPAD, Ibrahim Asane Mayaki. APRM ni mpango unaochagiza nchi za Afrika kujitathmini katika maeneo anuai ya kuboresha utawala bora katika nyanya za siasa, uchumi na maendeleo ya jamii na Tanzania ni miongoni mwa wanachama wake. Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib anayehudhuria mikutano ya APRM jijini Addis Ababa, kuimarika kwa Sekretarieti hiyo ya ngazi ya Bara kutachagiza kasi ya taasisi hiyo kuboresha utawala bora hapa Afrika hasa wakati huu Tanzania ikijiandaa kuwasilisha ripoti yake ya utekelezaji. APRM iliyoasisiwa miaka 10 iliyopita na Wakuu wa Nchi za Afrika kwa lengo la kuanzisha taasisi itakayokuwa na majukumu ya kufanya tathmini za mara kwa mara za hali ya utawala bora, tayari ni Mpango ambao hata Umoja wa Mataifa (UN) umeutaja kuwa ubunifu muhimu katika wakati huu Afrika ikiwa na changamoto nyingi za kiutawala, kiusalama na kisiasa. Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliwasilisha ripoti ya tathmini ya utawala bora nchi mwake katika kikao cha Januari, 2013 ambapo Tanzania ilisifiwa kuwa nchi ya mfano katika maeneo mengi ya kulinda usalama, utawala bora hasa katika siasa za maridhiano na Zaidi kuwa na mikakati
ambayo imesaidia ustahimilivu wa kisiasa, maendeleo ya kiuchumi na kijamii. “Tanzania ina mengi ya kuifunza Afrika. Afrika Kusini inajivunia sera nzuri za Tanzania zilizosaidia ukombozi wan chi yetu na tuko tayari kuja kujifunza Zaidi namna ya kuendesha demokrasia,” alikaririwa Rais Jacob Zuma alipokuwa akitoa maoni yake baada ya ripoti ya Tanzania kujadiliwa. Kwa mujibu wa Mtendaji wa APRM Tanzania mbali ya kuteuliwa bosi huyo mpya wa APRM, taasisi hiyo pia imempokea mwanachama mpya ambaye ni Ivory Coast iliyojiunga kama ishara ya kuonesha utayari wake wa kufanyiwa tathmini na wanachama wenzake na pia viongozi hao walitangaza nafasi mbalimbali za watendaji wengine waandamizi walioteuliwa.