CHAMA cha ANC kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika Jumatano ya wiki iliyopita. Tume ya uchaguzi nchini Afrika kusini imetangaza matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu huo na kusema kuwa chama tawala cha ANC kimejipatia ushindi mkubwa wa asilimia 62.
Katika hotuba yake kwa taifa Rais jacob Zuma amesema kuwa matokeo hayo ni ishara njema kwamba raia nchini humo wana imani na chama cha ANC na kwamba chama hicho kitatumia umaarufu wake kuimarisha maisha ya watu masikini nchini humo. Alisema kuwa ushindi huo umeipa serikali yake uwezo wa kuimarisha ukuwaji wa uchumi pamoja na ubunifu wa ajira.
Chama hicho ambacho kimekuwepo madarakani kwa miaka 20 sasa tangu kukamilika enzi za ubaguzi wa rangi nchini humo kinamhakikishia Rais Jacob Zuma muhula wa pili madarakani licha ya kuzongwa na kashfa mbalimbali. Huu ni uchaguzi wa bunge wa kwanza ambapo vijana walozaliwa baada ya kumalizika utawala wa ubaguzi, wameshiriki.
-BBC