AMREF Wampa Tuzo ya Ubalozi Mama Salma Kikwete

Mke wa Rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete

Mke wa Rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kuwa balozi wa kampeni ya Simama kwa ajili ya mwanamke wa Afrika “Stand for African Mother campaign” kwa ajili ya kujitoa kwake na kuwahamasisha wake wa Marais wa Afrika kusimama na kupigania haki za kina mama na watoto.

Hafla fupi ya kukabidhi tuzo hiyo ambayo imetolewa na Taasisi inayoshughulika na masuala ya Afya Afrika (AMREF) ilifanyika katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo jijini Dar es Salaam.

Akiongea kabla ya kukabidhi tuzo hiyo Mkurugenzi mkazi wa AMREF Dkt. Festus Ilako alimpongeza  Mama Kikwete kwa kazi anayoifanya ya kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua nchini.

“Tangu kuzinduliwa kwa kampeni hii mwaka 2012 tumefanikiwa kusomesha wakunga 250 hii ni karibu na asilimia 10 ya wakunga ambao wanatakiwa kusomeshwa katika kampeni hii.

Changamoto kubwa inayotukabili ni kutokuwa na fedha za  kutosha za kuwasomesha wakunga hawa lakini naamini ifikapo mwaka 2016 malengo yetu yatatimia”, alisema Dkt. Ilako.

Alisema mkunga mmoja anaweza kuwahudumia wanawake 5000 kwa mwaka, kama watu wataweza kulipia mafunzo ya wakunga idadi yao itaongezeka na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.

Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA aliwashukuru AMREF kwa tuzo waliyompatia na kusema kuwa siyo kama yeye ni hodari sana bali ni kutokana na kujitoa kwake kushiriki na kupigania mambo mbalimbali yahusuyo wanawake.

Mama Kikwete alisema, “Ukimwezesha mwanamke mmoja umeiwezesha familia nzima pia mwanamke akiamua kuiinua au kutoiinua familia yake anaweza kufanya hivyo jambo la muhimu ni kumsaidia ili aweze kupata elimu ambayo itamsaidia kuepukana na ujinga, maradhi na umaskini jambo ambalo litasaidia kupunguza na kufikia sifuri vifo vya wamama wajawazito na watoto”.

Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwataka AMREF wajipange na kuweka maadhimio yao ili waweze kuongeza kasi zaidi ya kuwasomesha wakunga na kuweza kuvuka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 30 kwa mwaka.

Mama Kikwete aliwahimiza wake wa marais wa Afrika kuunga mkono kampeni ya AMREF ya kuwasomesha wakunga 15000  barani Afrika ili kupata wataalamu wengi zaidi ambao watawahudumia kina mama wajawazito wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza vifo vyao na vya watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi katika mkutano wao uliofanyika mwezi wa tano mwaka 2013 makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa nchi mbalimbali Duniani nchini Tanzania ilizinduliwa na Mama Kikwete mwishoni mwa mwaka 2012 katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam huku ikiwa na malengo ya kusomesha wakunga 3800 hadi kufikia mwaka 2016.
Mwisho.