HUKU zoezi la upigaji kura likikaribia kuanza nchini Kenya, wagombea viti mbalimbali wamehimizwa kuzingatia kanuni za uchaguzi na kukubali matokeo ya uchaguzi huo ili kuepukana na kutokea kwa ghasia. Wito huo umetolea na kundi la waangalizi wa uchaguzi linalojiita “Group of Concerned Kenyans Initiative.”Kwenye mkutano na waandishi wa habari, kundi hilo likiongozwa na mwenyekiti wake, Generali Daniel Opande limesema limeridhishwa na matayarisho ambayo yamefanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC na kwamba wakenya walipata funzo kutokana na uchaguzi uliopita wa mwaka 2007.
“Tuna imani kwamba tume ya uchgaguzi IEBC itasimamia uchaguzi utakaokubaliwa na wote. Kwa maini yetu nikwamba mifumo ya kusuluhisha mizozo iko tayari na Jaji Mkuu ametuhakikishia kwamba idaya yake ya mahakama iko tayari kushughulikia kesi zote zitakazowasilishwa baada ya uchaguzi huo,” amesema Jenerali Opende.
Ujumbe wa kuhimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wao umetawala maeneo mbalimbali. Kundi hilo la wachunguzi limetoa mwito kwa vyombo vya habari kuwajibika katika ripoti zao ili kuepusha ghasia. Waangalizi hao wametoa mwito kwa rais atakayechaguliwa kwenye uchaguzi huo wa kesho kuwajumuisha wakenya wote kwenye serikali yake bila kujali ni nani alimpiga kura au ni yupi hakumchagua ili kuleta amani nchini.
Na katika maeneo mengine nchini humo, viongozi wa dini wamkuwa wakitoa mahubiri ya kuhimiza amani wakati na baada ya uchaguzi huo. Katika Kanisa la Kivanjisti la mjini Nairobi, Wainjilisti watatu walibadilishana zamu za kuyamuagia sifa baadhi ya makabila. Wakikuyu walisifiwa kwa kuwa wajasiriamali, Waluo kwa kuthamini elimu na Wakalenjini kwa kuwa watiifu. Uhuru Kenyatta kutoka kabila la Kikuyu, na Raila Odinga ambaye ni Mluo, ndiyo wagombea wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.
Mikutano ya kampeni ilihitimishwa siku ya Jumamosi, na wengi katika taifa hilo lenye wakristu wengi walielekea katika makanisa yao kufanya ibada, kuombea uchaguzi wa Jumatatu uwe wa amani, na kutoligawa taifa hilo kwa misingi ya kikabila, kama ilivotokea mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,200 waliuawa. Tayari waangalizi 36 wa Muungano wa Ulaya, 60 kutoka Umoja wa Afrika, na 40 wa Jumuia ya Afrika Mashariki wametawanyika kote nchini kwa shughuli hiyo ya uchaguzi inayoanza leo Jumatatu asubuhi.
-DW