Aliyebaka Mwanafunzi Darasa la Nne Ahukumia Miaka 30

Jaji Mkuu Tanzania, Chande Othuman

Jaji Mkuu Tanzania, Chande Othuman


Yohane Gervas, Rombo

MAHAKAMA ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro imemhukumu kifungo cha miaka 30, Philipo Mbiti (38) baada yakupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne. Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Rombo, Naomi Mwerinde alisema mahakama imemtia hatiani baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, ambapo upande wa mashtaka umedhibitisha pasipo shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Aidha alisema mtuhumiwa huyo ilidaiwa kutenda kosa hilo mnamo Novemba Mosi, 2013 katika eneo la Holili, Tarafa ya Mengwe, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kinyume na Sheria kifungu cha 130(2)e na 131 (1) sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kosa la ubakaji. Pia imedaiwa kuwa ushahidi uliowasilishwa na daktari umeonesha kuwa mlalamikaji aliumizwa vibaya katika sehemu zake za siri.

Awali upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na kitendo hicho alichokifanya kwani ni cha kikatili kwa mwanafunzi huyo mdogo wa darasa la nne. Baada ya maelezo hayo hakimu Mwerinde alisema kuwa mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine kwani vitendo vya ubakaji vimezidi kushamiri katika Wilaya ya Rombo.