Ali Kiba apata ajali

Mwanamuziki Ali Kiba

Mororogo

MWIMBAJI Ali Kiba na wacheza shoo wake wamenusurika kufa baada ya kupata ajali mbaya katika eneo la Mikumi,wakitokea Mbeya kuelekeaJijini Dar es salaam, kwenye barabara kuu ya Morogoro-Iringa ambapo saba wamejeruhiwa na watatu kati yao kulazwa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia majeruhi hao wakiwa wamelazwa wadi namba moja ya hospitali hiyo ya mkoa, huku msanii Ali Kiba aliyekuwa akizunguka huku na huko hospitalini hapo kuwahudumia waliuojeruhiwa, akikataa kata kata kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari na kuzuia kupigwa picha na wanahabari waliojitokeza hospitalini
hapo.

Hata hivyo katika kuonekana kuwa Msanii huyo alikusudia ajali hiyo isijulikane wazi, waandishi wa habari walianza kuzuiwa kuingia ndani ya geti la hospitali ya Mkoa wa Morogoro na walinzi waliokuwa zamu, wakidai kuwa uongozi wa hospitali umekataa waandishi kuingia ndani, na baada ya waandishi hao kutishia kumjulisha mganga mkuu wa mkoa,
waliwaruhusu kuingia.

Aidha ndani ya hospitali, Ali Kiba pamoja na kuelimishwa umuhimu wa habari hizo kuwekwa wazi ili kuwaondoa hofu wapenzi wa muziki wake na ndugu jamaa na marafiki watakaopata taarifa zisizo sahihi, bado aliwapiga marufuku wasanii wake kutozungumza chochote na waandishi wa
habari.

Kutokana na hali hiyo,kila msanii aliyeulizwa wakati Ali KIba hayupo eneo lao, namna ajali hiyo ilivyotokea na alivyofika hospitalini hapo, alidai kuwa alikuwa amelala wakati ajali ikitokea na kukataa kutoa ushirikiano zaidi kwa hofu ya bosi wao kumuona kuwa ni kihere here.

Hata hivyo wasanii walioweza kuongea na waandishi wa habari, walidai walikuwa wakitokea Mkoani Mbeya kuwahi ndege ya saa tano asubuhi jijini Dar es salaam ili kuelekea Mkoani Mwanza kwenye onesho la Fiesta na walikuwa katika gari ndogo aina ya Kugan mali ya Ali Kiba, iliyokuwa ikiendeshwa na dereva wa kukodi ambaye jina lakewala namba za gari hiyo havijaweza kufahamika mara moja.

Majeruhi waliolazwa, mmoja amejeruhiwa vibaya sehemu za kichwani, na mkononi, huku wengine wawili ambao kidogo hali zao ni nafuu wakionekana kujeruhiwa zaidi maeneo ya usoni na mwingine miguuni.

Baadhi ya waliokuwa katika msafara huo ambao wengine wamejitambulisha kwa jina moja moja, mbali na Ali KIba, ni pamoja na Sadam, Simon,Emmanuel Elias, Nassoro Bakari, ambao haijaweza kujulikana mara moja kama kweli hayo ndio majina yao halisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Adolphina Chialo, alipohojiwa kwa njia ya simu, alikiri kutokea kwa ajali hiyo ingawa taarifa kamili za namna ajali hiyo ilivyotokea zilikuwa bado zinafuatiliwa na askari wake.