Mshambulizi wa Corinthians Alexandre Pato amesema kuwa Chelsea ndio makao yake mapya.
Pato aliyasema hayo huku dukuduku zikisema kuwa huenda anaelekea Stamford Bridge kwa mkopo.
Mshambulizi huyo wa zamani wa AC Milan, 26, aliwasili Uingereza jumatano usiku kwa majaribio kabla ya kutia sahihi mkataba wa muda hadi mwezi wa tano.
Chelsea haijasema lolote kuhusu habari hizo zinazomshirikisha Pato, ambaye amekuwa nchini Brazil kwa mkopo kwa misimu miwili.
“Natamani sana kuichezea Chelsea. Nahitaji kucheza. nafurahia sana uhamisho huu.” alisema Pato.
Pato alijiunga na Milan mwaka wa 2007 akiwa na umri wa miaka 17. Hata hivyo hakushamiri kama ilivyotarajiwa na ikambidi kurejea Brazil mwaka wa 2013.
Tayari amefunga mabao 10 katika mechi 25 alizoichezea Brazil, ijapokuwa mara ya mwisho alipoitwa katika kikosi cha taifa ilikuwa ni 2013.