Al-Shabaab Wamuua Mwanajeshi wa Kenya

KUNDI la Al-shabaab

KUNDI la Al-shabaab limesema kuwa limemuua mwanajeshi wa Kenya usiku wa Alhamisi, baada ya kumalizika kwa muda walitoa kwa serikali ya Kenya kuwaachia Waislamu wanaoshikiliwa kwa tuhuma za ugaidi.

Wanamgambo hao wa Al-Shabaab wamesema pia kuwa wanachelewesha mauaji ya mateka wengine watano kwa masaa 72. Januari 23 wapiganaji hao waliipa serikali ya Kenya muda wa wiki tatu kuwaachia huru wapiganaji wanaoshikiliwa nchini humo, lakini serikali ya Kenya ilikataa kujadiliana nao na ilisema haingetekeleza matakwa yao.

Kabla ya kutoa muda huo kwa serikali ya Kenya, wanamgambo hao walimuua mateka wa Ufaransa Denis Allex ili kulipiza unyanyasaji wa ufaransa dhidi ya Waislamu, pamoja na operesehni za kijeshi za nchi hiyo dhidi ya makundi ya wapiganaji wa Kiislamu, ikiwemo ya nchini Mali. Jeshi la Kenya limesema hakuna kati ya maafisa wake anayeaminika kushikiliwa na Al-Shabaab.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaielezea Al-Shabaab kama kundi linalozidi kuporomoka, lisilo na udhibiti wa maeneo makubwa kama ilivyokuwa huko nyuma, na kwamba siyo tishio tena kwa serikali ya Somalia au jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika huko, lakini bado lina uwezo wa kufanya mashambulizi ya hapa na pale.

Serikali mjini Nairobi ilituma wanajeshi wake ndani ya mipaka ya Somali kuwasaka al-Shabaab Oktoba mwaka 2011, baada ya kundi hilo kuwateka watalii kutoka nchi za Magharibi katika ardhi ya Kenya. Al-Shabaab imesema bado ipo nafasi ya kuwaachiwa kwa wafungwa watano, wanaohusisha wafanyakazi wawili wa serikali.

Katika taarifa yao ambamo walitaja jina la mwanajeshi waliemuua, waasi hao wamesema licha ya Mujahideen kufungua milango ya majadiliano na kutoa muda wa kutosha, serikali ya Kenya imeonyesha uzembe wa maksudi, na imeshindwa kuchua hatua zinazostahiki ili kuwanusuru raia wake. Eneo la tukio la shambulio la kigaidi mjini Kampala Uganda, Julai 11, 2010. Eneo la tukio la shambulio la kigaidi mjini Kampala Uganda, Julai 11, 2010.

Kenya inawashikilia washukiwa kadhaa kwa madai ya kuwa na uhusiano na kundi la Al-Shabaab na iliwakabidhi wengine kwa serikali ya Uganda kuhusiana na shambulio baya la kujitoa mhanga mwaka 2010 mjini Kampala lililouwa watu 76, ambalo Al-Shabaab walidai kuhusika nalo. Wanamgambo hao walisema katika saa 72 zizajo, wafungwa watano waliosalia watapoteza maisha yao kutokana na usaliti wa serikali, au watasherehekea msaada wa serikali na kufurahia tena uhuru wao.

Wapiganaji hao walitoa mkanda wa video wenye kichwa cha habari kisemacho: “Wafungwa wa kivita wa Kenya: Ujumbe wa mwisho,” ambao ulimuonyesha Mule Yesse Edward, kiongozi wa serikali ya mtaa na Fredrick Irungu ambaye ni mfanyakazi wa wizara ya Uhamiaji. Wote walitekwa Januari mwaka jana wakati wapiganaji hao walipovuka mpaka na kuingia nchini Kenya, na kushambulia kituo cha polisi katika County ya Wajir, na kuua maafisa kadhaa wa Polisi.

Vidio hiyo pia ilikuwa na picha za mnato za wafungwa wanne ambao hawakutambuliwa, waliyosemekana kuwa wakenya pia.

-DW