Na Joachim Mushi
TUHUMA za uchotaji wa fedha Dola za Marekani milioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyotua bungeni imeendelea kuitesa Serikali huku kukiwa na kila dalili ya kuibuka mazitoka katika tuhumwa hizo. Leo mjini Dodoma wabunge mbalimbali wamechachamaa na kuungana kwa pamoja wakitaka ripoti ya uchunguzi huo iwasilishwe bungeni ili wabunge waijadili na kuitolea uamuzi.
Hali ya kuibuka kwa hoja za wabunge kutaka kuijadili ripoti hiyo ilianza mapema asubuhi ambapo katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu Bungeni, alisimama Mbunge Moses Machali wa NCCR-Mageuzi ambapo alimtaka Waziri Mkuu atoe msimamo wa Serikali juu ya utata wa suala hilo.
Akijibu swali hilo Waziri Pinda alisema uchunguzi umekwisha fanyika juu ya suala hilo na sasa lipo kwenye Kiti cha Spika hivyo Nafahamu kuwa suala hili lipo mezani kwako na pengine tukapata muda wa kujua kilichomo lakini bado haininyimi nafasi kuzungumzia kidogo kujibu hili aliloliuliza,” alisema Waziri Pinda.
“Uchunguzi utatuambia kama upande wa Serikali kipo kiasi cha fedha ambacho kilitakiwa zilipwe zitafuataliwa zirejeshwe, na hata kama kuna watuwataonekana kufunja taratibu Serikali itawachukulia hatua. Takukuru akisema Pinda unahusika katika hili Pinda atapelekwa tu hakuna cha salia mtume…utakwenda tu,” alisema Pinda.
Akifafanua zaidi juu ya kuwepo kwa Barua ya Mahakama Kuu kuzuia bunge kujadili suala hilo kwa msingi wa kwamba lipo mahakamani, Waziri Pinda alisema kwa uelewa wake (kama mwanasheria) si vyema vyombo hivyo viwili kuingiliana katika utendaji wa kazi hivyo kushauri iachiwe mahakama ifanye kazi yake.
“…Mfumo na msingi wa utawala nchini si vema muhimili hii miwili kuingiliana,” alisisitiza Pinda na kuongeza kuwa hali hiyo ikitokea itatoa picha mbaya kwa vyombo hivyo. Hata hivyo wabunge wengi wakiwemo wa chama tawala walimpinga baadaye kwenye mjadala wakitaka suala hilo lijadiliwe bungeni na litolewe maamuzi na kama kuna watuhumiwa walikiuka taratibu na kujichotea mabilioni waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
Wabunge wengi waliozungumza walionekana kuchachamaa wakitaka Bunge lisiingiliwe ili lifanye kazi yake na hivyo kutaka ripoti hiyo ijadiliwe bungeni. Walisema Watanzania wanakamuliwa kuchangia ujenzi wa maabara na hasipitalini hakuna madawa ilhali kuna baadhi ya viongozi wanajichotea mabilioni ya fedha za Serikali na kujinufaisha wenyewe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema kamati yao ipo tayari kuwasilisha ripoti hiyo bungeni muda wowote itakapoitajika ili ijadiliwe wazi kabla ya kutolewa uamuzi. Alisema hatua hiyo itaonesha mbivu na mbichi juu ya tuhuma hizo kwa waongo kujulikana, waliohusika kujulikana hivyo kila mmoja kuwajibika kwa kosa lake.
Kiti cha Spika kiliwahakikishia wabunge kutenda haki juu ya suala hilo hivyo kuomba muda uongozi uliangalie zaidi. “…Hatuwezi kufanya umoja wa kulinda maovu, yaani sisi sote na nafasi zetu tuungane kulinda maovu,” alisema Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.
Ripoti ya sakata la uchotaji wa Dola za Marekani 200 milioni katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyotua bungeni wiki iliyopita, imeibua mambo mazito baada ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kugundua kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa mali ya Tanesco.
Taarifa zinaeleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya Tanesco kwa IPTL ni Sh321 bilioni, hivyo fedha zote za Escrow zilipaswa kwenda Tanesco na bado ingekuwa inadai. Ukaguzi wa akaunti hiyo uliamuliwa na Serikali baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kudai kuna ufisadi katika uchotaji wa fedha hizo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).