Na Janeth Mushi, Arusha
MFANYABIASHARA wa mjini hapa amefariki dunia baada ya
kupigwa, kukatwakatwa vibaya sehemu anuai za mwili na kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa kile kudaiwa kupora pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’.
Mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Lomayan Kisioki (37) mkazi wa eneo
la Kwa Pole, lililopo Kata ya Nduruama wilayani Arumeru mkoani hapa. Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa sita mchana katika soko lililopo eneo hilo, ambapo inadaiwa kuwa wakati mfanyabiashara huyo akiendelea na shughuli zake ghafla alivamiwa na kundi la watu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha Akili Mpwapwa akitoa
taarifa kwa vyombo vya habari jana alisema kuwa watu hao walipeleka
marehemu huyo pembeni mwa barabara na kuanza kumpiga.
Kaimu huyo alisema kuwa watu hao walimpiga mfanyabiashara huyo na
kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumchoma moto.
Akili alidai kuwa watu hao walidai kuwa siku za hivi karibuni Kisioki
alikodisha pikipiki iliyokuwa na namba za usajili T 613 BNF iliyokuwa
ikiendeshwa na Frank Simon (30).
Alisema kuwa baada ya kukodisha pikipiki hiyo marehemu alimvamia
mwendesha pikipiki hiyo na kumpora,ambapo mmiliki wa pikipiki hiyo ni
Akundaeli Nanyaro.
Mpwapwa alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha
kuhifadhi maiti katika hospitali ya mkoa ya Mt.Meru na upelelezi juu
ya tukio hilo unaendelea.