Akamatwa akimiliki duma kinyume cha sheria

Mnyama aina ya duma

Na Mwandishi Wetu
Arusha

KIKOSI cha Kupambana na Ujangili Kanda ya Kaskazini kinamshikilia Rahman Hassan kwa tuhuma za kupatikana na wanyama aina ya duma (Cheater), huku watatu akiwa amewaficha nyumbani kwake eneo la Sombetini Arusha.

Duma hao inadaiwa wamekamatwa na badhi ya wafanyabiashara maarufu katika Jiji la Arusha na inasadikiwa walikuwa wanasafirishwa kwenda nje ya nchi.

Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho Kanda ya Kaskazini, Charles Mvungi amesema juzi kuwa wanyama hao wametolewa kwenye mbuga zilizopo kati ya Terrat na Simanjiro, hata hivyo mume wa Rahman amedaiwa kukimbia na ni miongoni wa watu sita ambao wanatafutwa na kikosi hicho.

Kukamatwa kwa Rahman kunafuatia taarifa za wasamaria wema ambao walitoa taarifa katika kikosi na Machi 30 mwaka huu askari wa kikosi hicho walikwenda Sombetini na kuwakuta wanyama hao wakiwa katika masanduku matatu, wawili wakiwa majike na mmoja dume.

Mvungi amefafanua kwamba duma hao wanathamani ya dola za Kimarekani 10,500 sawa na sh. milioni 15, 802, 500 na hivi sasa kikosi kinaendelea kuwasaka watu waliohusika na kuwakamata duma hao na kusafirisha pamoja na mfanyabiashara mmoja maarufu wa mjini Arusha.

Kaimu Kamanda Mvungi amesema kwa sasa duma hao wako hatarini kutoweka mbugani kutokana na ongezeko la vitendo vya ujangili vinavyofanywa dhidi ya wanyama hao.

Alisema takwimu zinaonesha kuwepo na duma 569 kwa mwaka 2007 nchini, huku asilimia 60 ya duma hao wanapatikana nje ya maeneo ya hifadhi za Taifa.

Hata hivyo amesisitiza kuwa kwa mujibu wa taarifa za taasisi ya utafiti wa wanyama pori (TAWIRI) chini ya utafiti wa duma idadi ya duma utafiti bado unaendelea ili kujua idadi kamili ya duma Tanzania.

Aidha amedai taarifa zinaonesha kuwepo na duma kati ya 250 hadi 300 katika hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti pamoja na Ukanda wa Maasai Mara na kwamba kwa Bara la Afrika inakadiriwa kuwepo na duma 7,500 tu. Aliongeza kuwa inakadiriwa kuwepo na duma kati ya 9,000 hadi 12,000 maeneo mbalimbali duniani.

Mvungi ameeleza kuwa taarifa za uchunguzi kutoka kikosi hicho zimebaini kuwa miongoni mwa waliomo katika mtandao huo ni mfanyabiashara mmoja maarufu wa jijini Arusha anayeshirikiana na mtandao mmoja unaowasaka wanyama aina ya duma ambao wanasamani kubwa.